YULE binti Melina (15) aliyeandikwa kwenye Gazeti la Uwazi toleo la Juni 17, mwaka huu kwa kichwa cha habari kisemacho; MTOTO ATESWA SIKU 730 amedaiwa kutoroshwa na kupelekwa kusikojulikana.
Binti huyo aliyekuwa akifanya kazi za ndani ‘hausigeli,’ alidaiwa kuteswa na bosi wake aliyejulikana kwa jina la Yasinta Rwechungura, mkazi wa Boko Magengeni jijini Dar ambaye alifikishwa kwenye Makahama ya Wilaya Kinondoni, Dar kwa madai ya kumtesa mtoto huyo na kumsababishia majeraha.
Kutoroshwa kwa binti huyo kunadaiwa kutokea wiki chache baada ya binti huyo kumaliza matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar alipokuwa akiuguza majeraha.
Chanzo cha ndani kinadai kuwa mara baada ya mtoto huyo kuruhusiwa kutoka hospitalini, alikutana na baba yake aliyefika jijini Dar kutokea Kagera kwa ajili ya kusikiliza kesi ya mwanaye na kuanzia hapo mtoto huyo hajaonekana tena hali iliyotafsiriwa kuwa ametoroshwa.
....akionyesha majeraha aliyoyapata.
Wakizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita, wanaharakati waliojitambulisha kwa jina la Wanawake Katika Juhudi za Kimaendeleo walisema walibaini kuwa mtoto huyo ametoroshwa baada ya kumtafuta kwa muda mrefu ambapo waliwasiliana na ndugu zake ambao walisema Melina yupo Kagera na alipelekwa na baba yake.“Tulipowasiliana na ndugu zake walisema Melina yupo kijijini Ishozi- Kiziba, Kagera na tulipowauliza kwa nini amesafirishwa kimyakimya bila kuwahusisha wanaharakati, walisema kuna makubaliano yalifanyika,” alisema mmoja wa wanaharakati hao.
Kesi ya bosi wa Melina ilitajwa mara ya mwisho Julai 11, mwaka huu huku ikitarajiwa kusikilizwa tena Julai 29, mwaka huu katika mahakama hiyo.