Friday, August 15, 2014

EBOLA: HOSPITALI ZOTE ZAAGIZWA KUTENGA MAENEO MAALUMU


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid ameziagiza hospitali za mikoa na wilaya zote nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa ebola ikiwa ni maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Hatua hiyo imekuja baada ya ugonjwa huo kuendelea kuua mamia ya watu katika nchi za Magharibi mwa Afrika.
Dk Rashid alisema hayo jana muda mfupi baada ya kuzindua Ripoti ya Wakunga ya mwaka huu iliyoandaliwa na wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).
Alisema ni muhimu kwa hospitali za mikoa na wilaya kufanya maandalizi ya kina hata kama hatua za kudhibiti ugonjwa huo zinafanywa na Serikali.
“Ni kweli tumechukua tahadhari kukabiliana na ugonjwa huo lakini ni muhimu kutenga maeneo kwa ajili ya tiba. Ninaagiza hospitali za mikoa na wilaya kutenga maeneo ili kujiandaa, ”alisema Dk Rashid.
Ugonjwa wa ebola umeshaua watu 1,013 katika nchi za Liberia, Nigeria Guinea na Sierra Leone na watu 1,848 wakiwa wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Wilaya ya Temeke ndizo zilizotengwa kuhudumia ugonjwa wa ebola endapo utajitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Dk Rashid alisema pamoja na kwamba hadi sasa hakuna mgonjwa wa ebola aliyethibitika nchini, hatua za kila aina zinapaswa kuchukuliwa kama tahadhari.
Kuhusu ripoti hiyo, waziri huyo alisema Tanzania inahitaji wakunga waliopata mafunzo ili kuwasaidia wanawake kujifunga salama.
Alisema asilimia 50 ya wanawake wanajifungua nje ya hospitali hasa vijijini hivyo msaada wa wakunga unahitajika kwa kiwango kikubwa.
Mtaalamu wa Mipango wa Mifumo ya Afya wa UNFPA, Felister Bwana alitoa wito kwa Serikali kuhamasisha vijana kujiunga na taaluma ya ukunga na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya afya ili kuongeza idadi wauguzi na wakunga.