Tuesday, August 12, 2014

KAVUMBANGU AINUSURU AZAM KULALA KWA WASUDAN

AZAM FC imepunguzwa kasi katika Kombe la Kagame, baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Atlabara ya Sudan Kusini jioni hii Uwanja wa Stade de Kigali, Nyamirambo mjini hapa.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Didier Kavumbangu aliinusuru Azam kuzama katika mchezo huo wa Kundi A Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 86, baada ya krosi ya Shomary Kapombe.

Mkombozi; Didier Kavumbangu ameifungia bao la kusawazisha Azam FC leo Kigali

Azam ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Kipre Michael Balou kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20, baada ya pacha wake, Kipre Herman Tchetche kuangushwa.
Atlabara ilirudi vizuri kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 48, mfungaji Nahodha wake, Thomas Batista kabla ya kufunga la pili dakika ya 60 mfungaji Bony Martin. 
Atlabara ilipata pigo dakika ya 89 baada ya Nahodha wake, Batista kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Shomary Kapombe akiruka kwenda chini baada ya kuchezewa rafu na beki wa Atlabara

Kwa matokeo hayo, Azam inafikisha pointi tano baada ya mechi tatu na kujihakikishia nafasi ya kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo, wakati Atlabara inafikisha pointi mbili baada ya mechi mbili.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Gardiel Michael, Shomary Kapombe, Said Mourad, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Gaudence Mwaikimba/Didier Kavumbangu dk63, Leonel Saint Preux na Kipre Tchetche/Khamis Mcha dk63. 
Atlabara; Jacko Mpenzi, Thomas Batista, Hamza Olema, Hatit Monydeng, Ibrahim Sebit, Kharim Mutawakil, Frando Justin Wani, Joseph Aquer, Dak Kujbor/Khamis Leon dk56 na Bony Martin.