Wednesday, September 3, 2014

AJA, JAJA, JAJA…YANGA WAWAAA, WAKENYA CHALI TAIFA

BAO pekee la Mbrazil Genilson Santana Santos ‘Jaja’ limeipa Yanga SC ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Thika United ya Kenya katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Jaja alifunga dakika ya 58 kwa pasi ya Simon Msuva na hilo linakuwa bao la pili kwa Jaja tangu ajiunge na Yanga SC miezi miwili iliyopita, akiwa amecheza mechi yake ya nne leo. 
Shujaa wa leo; Genilson Santana 'Santana' akishangilia baada ya kufunga bao pekee leo

Jaja aliingia ‘mzima mzima’ pembezoni mwa lango la Thika kuhakikisha anaiunganishia nyavuni krosi ya Msuva kwa vyovyote na akafanikiwa akimuacha kipa Mganda, Hamza Muwonge anaokota mpira nyavuni.
Kwa furaha ya bao hilo, Jaja ambaye alikuwa akizomewa na mashabiki wa Simba SC kila alipokosea alitoka nje ya Uwanja kushangilia bao hilo, kwa shangwe za aina zote alizoweza.
Yanga SC haikucheza vizuri kipindi cha kwanza na zaidi ilitegemea kupitisha mashambulizi yake pembeni walipokuwa wakiteleza kwa awamu Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Andrey Coutinho.
Coutinho alikaribia kufunga mara mbili kwa mipira ya adhabu aliyopiga kutoka nje kidogo ya eneo la penalti, wakati Jaja hakuwa na madhara kabisa kipindi cha kwanza.
Nafasi nzuri zaidi kwa Thika ilikuwa dakika ya 20 wakati shuti la Moses Odhiambo lilipodakwa na kipa Deo Munishi ‘Dida’- zaidi ya hapo, safu ya ulinzi ya Yanga SC leo ilicheza vizuri.
Kipindi cha pili, kocha Mbrazil Marcio Maximo alianza na mabadiliko katika safu ya kiungo akimpumzisha Hassan Dilunga na kumuingiza Hamisi Thabit, ambaye alikwenda kuibadilisha timu.
Penaaalti; Kiungo Andrey Coutinho akienda chini baada ya kuchezewa rafu na beki wa Thika, lakini refa Hashim Abdallah hakutoa penalti

Angalau Yanga wakaanza kucheza mpira, pasi zilionekana kutembea uwanjani na mashabiki wakaanza kushangilia ‘chama lao’.
Ni Hamisi Thabit ambaye alimpasia mpira mzuri Msuva, aliyemtoka beki wa Thika hadi nje kidogo ya eneo la penalti alipomtilia krosi Jaja, aliyefunga bao hilo pekee.
Refa Hashim Abdallah aligoma kutoa penalti dakika ya 62 baada Coutinho kuangushwa kwenye eneo la hatari, wakati Said Bahanuzi aliyetokea benchi alichelewa kuunganisha krosi nzuri ya Niyonzima dakika ya 80.  
Huo unakuwa mchezo wa nne kwa Maximo tangu aanze kazi Yanga SC Julai mwaka huu na amefanikiwa kushinda mechi zote, 1-0 dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani, Pemba kabla ya kushinda 2-0 mara mbili dhidi ya Shangani na KMKM Uwanja wa Amaan, Zanzibar. 
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga/Hamisi Thabit dk46, Haruna Niyonzima/Omega Seme dk73, Genilson Santana ‘Jaja’/Said Bahanuzi dk87, Andery Coutinho/Nizar Khalfan dk60 na Simon Msuva/Hussein Javu dk70.
Coutinho ameendelea kung'ara Yanga SC
Share T