Wednesday, September 24, 2014

ULINZI WAIMARISHWA MARA DUFU BUNGENI


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kuleta kiwewe ndani ya Bunge la Katiba ambako sasa ulinzi umeonekana kuongezwa mara dufu.
Wakati wote kumekuwa na simulizi ya ulinzi ulioimarishwa katika viwanja vya Bunge la Katiba tangu kuanza kwake Februari 18, mwaka huu, ingawa kwa sasa umeongezeka mara dufu.
Tangu Chadema walipotangaza nia yao ya kufanya maandamano ya kupinga kuendelea kwa Bunge hilo, vyombo vya ulinzi viliweka mkakati wa kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kupenya na kulifikia jengo hilo bila kibali maalumu.
Jana, Polisi waliongeza umbali wa ulinzi katika kulifikia jengo la Bunge na hakuna gari wala mtu aliyeweza kuwapita polisi hao bila ya kukaguliwa na kuulizwa vibali.
Kwa muktadha huo, ili kufikia sehemu ya ukumbi wa Bunge, kulimlazimu mtu kama mwandishi wa Habari kuvuka vizuizi vitatu ndipo afike sehemu ya kufanyia kazi zake.