Monday, October 20, 2014

FIESTA 2014: KAMA NOMA NA IWE NOMA!

Kama noma na iwe noma! Tamasha la Serengeti Fiesta 2014, wikiendi iliyopita lilifunga mitaa ya Jiji la Dar na viunga vyake ambapo burudani ya kufa mtu ilidondoshwa kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar na kugubikwa na matukio kibao nyuma ya pazia, likiwemo la msanii kutoka Nigeria, Davido ‘kupafomu’ pamoja na serikali kumkataza, Ijumaa Wikienda lina ripoti kamili.
Nyomi ya watu ikiwa imefurika Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar kumshuhudia T.I katika Tamasha la Serengeti Fiesta 2014
SHUGHULI YAANZA
Shughuli ilianza kwa madansa ‘kusheki’ ambapo Kundi la Makomando ndilo lililoanzisha makamuzi na kupokea shangwe kubwa.
Baada ya Makomando, Wanaume TMK wakiongozwa na Chegge na Temba ndiyo waliofuatia, wakapiga shoo hevi na kupokea shangwe kubwa.
Msanii kutoka Nigeria, David Adedeji Adeleke 'Davido' akitoa burudani kwenye Tamasha la Serengeti Fiesta 2014 ndani ya Ledears Club.
Madee na Dogo Janja walipafomu pamoja baada ya kitambo kirefu tangu walipogombana,
Vanessa Mdee akafuatia na kunogesha na madansa wake kwa zogoazogoa, akaja Ommy Dimpoz ambaye naye alikamua kisawasawa bonge la shoo.
Msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz akitumbuiza kwa staili yake kwenye jukwaa la Serengeti Fiesta 2014 Dar Leaders.
SAPRAIZI YA DIMPOZ
Kwa mara ya kwanza, Ommy Dimpoz alitambulisha remix ya wimbo wake wa Tupogo kwa mahadhi ya mnanda au mchiriku ambapo yeye na madansa wake waliserebuka kinoma wakishirikiana na Msaga Sumu.
Msanii wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee akifana yake na Ommy Dimpoz.
YOUNG KILLER, BANANA ZORRO NAO JUKWAANI
Baada ya hapo, mtu mzima Banana Zorro alivamia jukwaa akiwa na Young Killer na Umebadilika ambapo nao walipokelewa vizuri na nyomi iliyokuwa imefunga uwanjani kabla ya Young Killer kubaki mwenyewe na kukisanua ileile.
Msanii Waje kutoka Nigeria akitoa shoo.
MSANII KUTOKA DUBAI MH!
Msanii wa kwanza mgeni kupanda stejini alikuwa Ash Hamman kutoka Dubai ambaye ngoma zake hazikuwa zikijulikana kiivyo.
ZAMU YA WAJE KUTOKA NIGERIA
Msanii wa pili mgeni alikuwa ni Waje kutoka Nigeria ambaye alianza kwa kufundishwa kutamka maneno ya Kiswahili yakiwemo ‘nipeleke nyumbani’ ambaye kimavazi aliacha maswali kwa kuvaa kisweta cha aina.
Msanii huyo alimpagawisha Madam Rita na kujikuta akishindwa kujizuia, akaserebuka na kinywaji chake mkononi.
Msanii kutoka, Kenya Victoria Kimani akipagawisha mashabiki jukwaani.
VICTORIA KIMANI
Msanii wa tatu kutoka nje alikuwa ni Victoria Kimani wa Kenya ambaye aligonga ngoma zake mbili lakini kilichoonekana ni kwamba zilikuwa hazijulikani na wengi pamoja na kwamba alipata shangwe kimtindo.
Mwingine wa kimataifa alikuwa ni Bob Man wa Nigeria ambaye alipagawisha kwa reggae baada ya kupiga akapela ya Wimbo wa One Love wa Bob Marley huku akichombeza na maneno ya Kiswahili kama ‘mambo vipi’ na ‘nakupenda’. Alipojaribu kuwasifia warembo wa Kibongo, masela wakamaindi kidizaini fulani.
Bob Man aliendelea kufanya yake akisaidiwa na Victoria Kimani, wakakamua Prokoto ambapo Dimpoz aliungana nao, shangwe zikazidi kupamba moto.
Burudani ilizidi kukolea, akapanda mtangazaji na msanii wa Bongo Fleva, Adam Mchomvu ambaye alikamua kwa sana.
Msanii zao la THT, Rachel akikamua stejini na mashabiki zake
RACHEL, WACHEZA SHOO WAKE WAVAMIA JUKWAA
Msanii zao la THT, Rachel naye alipanda jukwaani na mashabiki wake sita waliokuwa wamevalia nguo zinazofanana, wakakamua ngoma yake ya Nashukuru Umerudi, na nyingine kibao lakini mashabiki walipooza kimtindo kwani nyimbo zake zilikuwa na mzuka wa chini, ikafuatia ngoma nyingine ya Umependeza, mashabiki kwa mbali wakaanza kuamka.
Recho akitumbuiza katika Tamasha la Fiesta.
BARNABA NA SHAA NAO WAPANDA JUKWAANI
Msanii mwingine, Barnaba Elias ‘Barnaba Boy’ naye alifuatia na ngoma yake mpya ya Wahalade, nyomi ikaamka na shangwe zikaanza kuonekana kutoka kila upande, akafuatia Shaa ambaye alitoa kali baada ya kutaka aitwe Mrs MJ (Master Jay).
Msanii Shaa akiendelea na makamuzi ndani ya Viwanja vya Leaders Kinondoni.
Ikafuatia burudani ya nguvu kutoka kwake ambapo alikamua Wimbo wa Lover Lover, ukaamsha popo, ukafuatia Promise, mashabiki wakazidi kuchangamka huku wacheza shoo wa msanii huyo nao wakizikonga nyoyo za mashabiki.Akaendeleza makamuzi, akafanya Remix ya Hoi iliyowakumbusha watu mbali, akamalizia na Sugua Gaga iliyobamba vibaya.
Msanii wa Bongo Fleva, Linah Sanga akilishambulia jukwaa.
NYANDU TOZ, BLU NOMA SANA
Msanii Nyandu Toz naye alifuatia jukwaani akipigwa tafu na Blu na memba wengine wa Micharazo, wakapata shangwe ya kufa mtu. Blu akabaki peke yake jukwaani, akakamua kinoma. Baada yake, walipanda jukwaani Yamoto Band, watu wakachangamkia makamuzi yao ile mbaya.
Msanii wa kitambo Mwana FA akikamua ngoma zake kali stejini.
MWANA FA ADHIHIRISHA UKONGWE WAKE
Mwana FA naye alipanda kwa staili ya kipekee, ngoma zake mpya na za kitambo zikawabamba mashabiki ile mbaya.
Mtangazaji Godwin Gondwe aliushtua umati uliokuwepo uwanjani hapo ambapo alisikika akitangaza taarifa ya habari ya dharura (breaking news), watu wakakaa mkao wa kusikia kilichojiri, kumbe anampandisha Stamina, akakamua kinoma na kupishana na Nay.
Staa wa Bongo Fleva, Emanuel Elibariki 'Nay wa Mitego' akitumbuiza katika Tamasha la Fiesta.
DIAMOND, ALI KIBA KAMA SIMBA NA YANGA
Muda uliwadia ambapo watangazaji mayanki wa Clouds FM, Hamis Mandi ‘B12’ na Dj Fetty walipanda jukwaani na kuanza kuwauliza mashabiki nani mkali kati ya Diamond na Ali Kiba, watu wote wakajibu: Kibaa! Kibaa!
Mkali wa ngoma ya Mwana, Ali Kiba na Mdogo wake Abdu Kiba wakikonga nyoyo za mashabiki stejini.
Wakauliza tena nani mkali kati ya Simba na Yanga, kila mmoja akatoa jibu lake.
ALI KIBA KWA STEJI
Mkali wa ngoma ya Mwana, Ali Kiba alipanda jukwaani, akapokelewa na shangwe la kufa mtu ambapo kwa upande wa mastaa, Rose Ndauka, Dida, Jack Pentzel na mumewe walimshangilia Ali Kiba kinoma, Halima Kimwana na Aunt Ezekiel wao walikuwa tofauti kabisa na Ali Kiba, walikuwa wakimsubiri Diamond.
Ali Kiba alifanya makubwa jukwaani, katikati kiliingia kibwagizo ambapo kiti cha kifalme kilifutwa vumbi, Ali Kiba akakikalia na kuvalishwa taji la ufalme, maneno ya The Return of The King yakakisindikiza kibwagizo hicho, ikafuatia ngoma ya Mwana iliyomaliza ubishi, mpaka anashuka jukwaani, bado mashabiki walionekana kuwa na kiu kubwa.
Kundi la weusi likiwakilisha.
LINAH, WEUSI NI SHEEDAH!
Baada ya hapo, msanii zao la nyumba ya vipaji Tanzania, Esterlina Sanga ‘Linah’ aliyekuwa ametinga kivazi ‘chenye hoja’ alipanda jukwaani, akafunika mbaya na ngoma zake kali ikiwemo Ole Themba, wacheza shoo wake kibao wakakamua ile mbaya kitamaduni na kuchangamsha shoo nzima. Walifuatia Weusi waliopanda na sapraizi ya kupanda jukwaani kwa msanii Lord Eyez, makamuzi ya kigumu yakaendelea ambapo wakali kibao wakiongozwa na Joh Makini walifanya yao, uwanja wote ukalipuka kwa shangwe ya nguvu kwa muda mrefu.
Diamond Platinumz na Davido wakionyesha umahiri jukwaani.
DIAMOND AAAH WAPI!
Ilifuatia zamu ya mkali wa ngoma ya Mdogomdogo, Diamond Platinumz ambapo mashabiki wake walitangulia, akafuatia Diamond ambapo aliimba Remix ya Uswazi Take Away na Chegge, kombati zikazagaa jukwaani hata alipopanda Nay wa Mitego kumsindikiza kwenye ngoma ya Muziki Gani. Hata hivyo, shangwe hazikuwa kiivyo kama kwa Ali Kiba, akaendelea kukamua ngoma kibao lakini cha ajabu wakati akiendelea na shoo, zilianza kusikika kelele za kumtaja Ali Kiba, mpaka mchizi anamaliza, zomeazomea zilikuwa zikisikika chini kwa chini.
Staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Juma 'Diamond' akikamua jukwaani.
DAVIDO KAMA NONA NA IWE NOMA!
Licha ya mahakama kumzuia Davido kufanya shoo kutokana na matatizo ya kimkataba, waandaaji wa shoo hiyo, Clouds Media Group walimpandisha kuashiria kama noma na iwe noma na kuifanya serikali iduwae, harufu ya vita kati ya waandaaji na serikali ikaanza kunukia. Jina la Davido lilipotangazwa, tofauti na wasanii wengine, ilimchukua zaidi ya dakika nne kupanda jukwaani, akaibuka na kuanza makamuzi.
Hata hivyo, bado hakupata shangwe za nguvu kama ilivyotegemewa, akaimba nyimbo ambazo hazijulikani na wengi.
Mkali T.I, rapa kutoka nchini Marekani akifunga Shoo kwa makamuzi makali hadi naiti kali.
'Hata alipopanda Diamond kukamua naye Number One Remix, mambo yalikuwa ni yaleyale, hakukuwa na shangwe kama ilivyotegemewa. Kwa mbali watu walionekana kuamka alipokamua Skelewu na kumalizia na Aye.
Rapa kutoka nchini Marekani, Clifford Harris,'T.I' akitoa burudani kwenye tamasha la Fiesta Leaders Club jijini Dar .
T.I JUKWAANI
Mkali T.I, rapa kutoka nchini Marekani aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu, alidondoka jukwaani na kukamua ngoma zake kibao pamoja na zile alizoshirikishwa, amshaamsha zikatawala mwanzo mwisho na kuhitimisha msimu wa burudani wa Serengeti Fiesta 2014. Ilikuwa ni sheeeda!