Wednesday, October 8, 2014

HAWA NDIO MASTAA WALIJITOA BONGO MUVI




 Msanii wa filamu Bongo, Halima Yahya ‘Davina’.
HALI bado tete! Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Klabu ya Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ kujiuzulu, upepo mbaya unaendelea kuitafuna klabu hiyo ambapo sasa wasanii wengine watano wamejiengua, Risasi Mchanganyiko linakupa mchapo kamili. 
Kutokana na wasanii hao kujitoa, klabu hiyo inaonekana kupoteza muelekeo ambapo kwa sasa wanachama waliobaki kundini wanajipanga upya ili kuisimamisha upya.
Kwa mujibu wa chanzo makini, wasanii waliojiengua ni Halima Yahya ‘Davina’, Esha Buheti, Kajala Masanja, Flora Mvungi na  Salma Salmini ‘Sandra’ huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kukithiri kwa vitendo vya ngono na ubaguzi wa kimaslahi.
 
Msanii wa filamu Bongo, Flora Mvungi akipozi.
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ubuyu kwamba, hivi karibuni kulitokea safari ya wasanii kwenda mkoani Tanga lakini baadhi ya viongozi wamedaiwa kujichagua kwa ‘kapo’ bila kujali kuwa wapo wanachama wengine ambao wanatakiwa kwenda huko.
Kikifafanua madai hayo, chanzo hicho kilikwenda mbele zaidi na kuzinadi kapo hizo kama ifuatavyo:
Cloud 112 (Issa Musa) alidaiwa kuongozana na Coletha Raymond, JB (Jacob Steven) na Shamsa Ford, Rose Ndauka na Single Mtambalike (Rich) na wengine.
 
Msanii wa filamu Bongo, Kajala Masanja.
Baada ya madai hayo kutua kwa mapaparazi wetu, walianza kwa kuwatafuta walengwa ambao wamedaiwa kubaguliwa na kuamua kujitoa klabuni hapo. Mambo yalikuwa hivi:
Davina:
“Mimi nimeamua kujitoa kwa sababu naona mambo mazuri wanachaguana mapatna tu sisi tunakumbukwa pasipo mazuri, kwenye pesa wanapeana wao wenyewe, mimi mpaka mume wangu alikuwa akiniuliza kwamba napata faida gani.”
 
Msanii wa filamu Bongo, Salma Salmini ‘Sandra’
Sandra:
“Sijapata faida yoyote Bongo Movie, watu wanapeana mapatna inapotokea suala la safari na pesa.”
Esha Buheti:
“Mimi nimeamua kujitoa kwani watu wamekuwa na ubaguzi, sisi tunaitwa unapotokea msiba tu, nitafanya kazi zangu mdogomdogo, nitatoka tu.”
 
Msanii wa filamu Bongo, Esha Buheti.
Kajala:
“Nimejitoa kwa sababu kule nilikuwa nikimfuata Steve Nyerere, sasa ameshatoka nafuata nini tena?”  
Jitihada za kuwapata wasanii wanaotajwa kuwa ni wabaguzi ziligonga mwamba kwa baadhi ya wasanii lakini alipopatikana Cloud 112, alikanusha taarifa hizo.
“Hakuna kitu kama hicho, sisi tunasafiri kulingana na matakwa ya waandaaji wa safari, waandaaji ndiyo wanaosema wanamtaka nani katika shughuli yao, wanaosema hivyo wamekosa la kuongea,” alisema Cloud 112.