Thursday, October 16, 2014

MADAKTARI BINGWA AFRIKA KUSINI ‘WAMRUDISHA FASTA’ IVO KUDAKA SIMBA NA YANGA JUMAMOSI TAIFA

KIPA Ivo Mapunda ndiye anaweza kusimama kwenye lango la Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikimenyana na mahasimu, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ivo alifanyiwa vipimo nchini Afrika Kusini mapema wiki hii na tiba za kumuondolea maumivu kabisa, ili Jumamosi aweze kufanya kazi iliyomsababisha akasajiliwa Simba SC Desemba mwaka jana kutoka Gor Mahia.
Ivo alihitaji wiki nane za mapumziko baada ya kuumia kidole gumba mwisho mwa mwezi Septemba, lakini kutokana na kuumia kwa kipa wa pili, Hussein Sharrif ‘Cassilas’ amelazimika kufupisha muda wa mapumziko.

Kipa Ivo Mpaunda wakati anafanyiwa vipimo Afrika Kusini
Ivo akiwa anapimwa kidole chake gumba kilichoumia
Tangu ametua Johannesburg, Afrika Kusini Jumatatu wiki hii ambako Simba SC ilikuwa imeweka kambi tangu Oktoba 8, Ivo ambaye  atawasili mchana wa leo, baada ya vipimo na tiba alikuwa akifanya mazoezi ya nguvu, lakini si kudaka zaidi ya kurusha rusha mipira.
Fiziki ya mwili iko sawa kwa Ivo kwa sababu alipoumia kidole alipumzika wiki mbili tu na baada ya hapo akaanza mazoezi ya kukimbia na kujitupa tupa kama anachupia mipira.
Na baada ya tiba ya Madaktari bingwa Afrika Kusini, Ivo amekuwa akisema anajisikia vizuri- maana yake yuko tayari kuwazuilia michomo Yanga SC Jumamosi.
Kipa wa tatu, Peter Manyika aliyedaka mechi tatu baada ya Cassilas kuumia, akimalizia ya sare ya 0-0 na Orlando Pirates, ya kufungwa 4-2 na Bidvest Wits na 2-0 jana na Jomo Cosmos naye anaonekana kuwa vizuri kabisa.
Licha ya umri na uzoefu mdogo, lakini Manyika amejizolea sifa nyingi Afrika Kusini kutokana na udakaji wake mzuri katika mechi hizo tatu za kirafiki. 

-BIN ZUBEIRY