Tuesday, October 7, 2014

NOORAH, ASIMULIA TATIZO ALILOKUWA NALO AMBALO MADAKTARI WALISHANGAA IWEJE AWE HAI


Rapper Noorah aka Babastylez amesema kama isingekuwa neema za Mungu, leo hii asingekuwepo duniani.

Akiongea kwenye kipindi cha Siz Kitaa cha Clouds TV hivi karibuni, Noorah alidai alikuwa na tatizo la kujikunja kwa utumbo lililodumu kwa miaka 20. Amesema wakati tumbo likimuuma alikuwa akidhani ni vidonda vya tumbo.
 
“Doctor amekuja kunifanyia operesheni, baada ya operesheni akamuita mama pembeni. Akamwambia ‘mama huyu mwanao ana Mungu sana’. Maana kitu alichokikuta huko tumboni, hakuna binadamu anaweza akawa hai kwa hali ile. Utumbo wangu mdogo ulikuwa umejikunyata wote. Akauliza ‘alikuwa anapataje choo huyo!’"
 
Alisema operesheni hiyo ilidumu kwa masaa sita na ilifanyika kwenye hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam.
 
“Nimetoka dokta anasema utumbo wangu ulikuwa umekuwa mdogo kama wa mtoto mchanga kwahiyo ulikuwa unapitisha chakula kwa tabu sana. Kwahiyo kipindi hicho nilikuwa nakula vyakula vya kusaga tu, na vyenyewe sometimes vingine havipiti.”
 
Pamoja na kuwa amepona tatizo hilo, Noorah amesema ana tatizo jingine linalofanya awe anapata vitu kama vifafa (seizure) ambavyo vimesababisha na ajali aliyopata mwaka 2005 iliyomfanya apate tatizo kwenye ubongo.
 
 “Sasa hivi dokta ameshanipa treatment na ameniomba nije nipate mind rest,” alisema Noorah ambaye kwa sasa amerejea kwao Shinyanga kama sehemu ya maagizo ya wataalam.
 
Noorah aliwaasa wasanii na watu wengine kuwa na desturi ya kuchunguza afya zao mara kwa mara kubaini matatizo yanayowasumbua.