UKATILI! Watu wasiojulikana wameyakatisha maisha ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Mkwajuni, Kigamboni jijini Dar, Ibrahim Hamis (30).Tukio hilo la kusikitisha na lililowaacha midomo wazi wakazi wa eneo hilo, lilijiri usiku wa saa mbili hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita, mmoja wa viongozi wa chama hicho kutoka Shina Namba 13 Mkwajuni Vijibweni, Mrisho Bindo alisema siku ya tukio, marehemu alikuwa kwenye pikipiki akimpeleka mtu mahali.
Alisema baada ya kumfikisha mtu huyo eneo linaloitwa Mkorea, akiwa anarudi alitekwa na watu wasiojulikana na kumpotezea uhai kwa kumteka na kumuua kwa kumpiga na kitu kizito kichwani kisha kuchukua pikipiki yake na kutokomea kusikojulikana.
Bindo ambaye ni mjumbe wa shina huko Kigamboni aliongeza kuwa eneo alilofanyiwa ukatili marehemu lina hali mbaya kiusalama maana ni porini hasa kwa nyakati za usiku ni tatizo kwa wapita kwa miguu.
Katika msiba huo, diwani wa eneo hilo kupitia CCM, Suleiman Methew Luwongo alilaani vikali mauaji hayo ambayo yamekatisha uhai wa kiongozi huyo na kuiacha familia yake ikiwa haina cha kufanya.
Katika msiba huo, diwani wa eneo hilo kupitia CCM, Suleiman Methew Luwongo alilaani vikali mauaji hayo ambayo yamekatisha uhai wa kiongozi huyo na kuiacha familia yake ikiwa haina cha kufanya.
Aidha, aliomba eneo hilo ambalo hadi sasa limekaa kama pori wagawiwe watu ili waweze kuliendeleza kuliko maeneo hayo kutumika katika uporaji na mauaji kwa watu.‘’Ninaiomba serikali kupitia wizara husika kulifanyia utaratibu lile eneo ikiwa ni kulimilikisha kwa wakazi wa huko ili liendelezwe,’’ alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Kihenya wa Kihenya alitihibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema zoezi la kuwasaka watuhumiwa linaendelea.Marehemu alizikwa Oktoba 12, mwaka huu katika Makaburi ya Vijibweni, Kigamboni jijini Dar es Salaam.