SIKU chache baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangazwa kuwa anaongoza katika kinyang’anyiro cha urais 2015, mastaa mbalimbali wanaomuunga mkono wameandaa mkakati wa kumfanyia sherehe ya kumpongeza.
Chanzo makini kilichopo ndani ya kamati ya wasanii hao wa Bongo Movies, kitendo cha Taasisi ya Twaweza kutangaza kuwa Lowassa anaongoza na kuwagaragaza makada wenzake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwao ni ishara tosha ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.
“Mastaa wa Bongo Movies wanaomuunga mkono Lowassa wameandaa bonge la pati la kumpongeza Lowassa na siku hiyo watakula, watakunywa maana mipango yao tayari wanaona inakwenda vizuri na hakuna mtu ambaye anaweza kumuangusha katika chama hicho,” kilisema chanzo bila kutaja lini na wapi watakapofanyia sherehe hiyo.Staa katika tasnia ya filamu Bongo, Esha Buheti.
Mbali na sherehe hiyo kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali, chanzo hicho kimeeleza kuwa wanatarajiwa pia kualikwa wananchi mbalimbali wanaomuunga mkono Lowassa.
“Safari ya kuelekea uchaguzi mkuu ndiyo imeanza rasmi, Twaweza wametafiti na kubaini kile ambacho sisi tulikuwa tunakiamini, Lowassa hana mpinzani CCM, ushindi ni lazima,” kilisema chanzo hicho.
Wasanii ambao wanatajwa kuwa upande wa Lowassa ni Jacqueline Wolper, Esha Buheti, Mahsein Awadhi ‘Dk. Cheni’, Wema Sepetu ‘Madam’ na wengine kibao.
Taasisi ya Twaweza iliyofanya utafiti kwa mwezi Septemba, ilitangaza matokeo hayo Jumatano iliyopita na mtafiti wake, Elvis Mushi ambapo alisema wananchi 1,445 walihojiwa kwa njia ya simu ambapo Lowassa alipata asilimia 13 huku waziri mkuu wa sasa, Mizengo Pinda akimfuatia kwa kupata asilimia 12.
Wengine waliopigiwa kura katika utafiti huo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbrod Slaa aliyepata asilimia 11, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akipata asilimia 6 huku Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe akiondoka na asilimia 5.