Tuesday, November 18, 2014

MUHIMBILI VIFO NJE NJE KISA DAWA HAKUNA



Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’I
NATISHA! Uhaba mkubwa wa madawa, ongezeko la ada ya kitanda na chakula katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, umesababisha watu wengi kupoteza maisha kufuatia wagonjwa kukosa huduma na hivyo kurejea majumbani mwao.
Baadhi ya wagonjwa wakiwa katika moja ya wodi za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baada ya Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kusitisha kutoa dawa kwa hospitali hiyo kubwa ya serikali kufuatia deni kubwa, wagonjwa hasa wenye uwezo mdogo wamelazimika kuingia mitaani na kuombaomba kwa wasamaria wema ili waweze kunusuru hali zao.
Katika wodi ya wagonjwa wa moyo, walilalamikia bei kubwa ya matibabu inayowafanya wasio na uwezo na wasio na ndugu kuishi kwa kubahatisha. “Hali ni mbaya sana hapa, jana nimeshuhudia wagonjwa wenzetu wawili wanapoteza maisha kwa sababu hawahudumiwa tokea majuzi kwa vile hakuna dawa, na tunasikia hata huko katika mawodi mengine hali ni ya hatari kabisa,” alisema mgonjwa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Moja ya jengo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika wodi ya wazazi, kulikuwa na ukosefu wa vifaa tiba kama vile pampas na wagonjwa wengi walionekana kujirundika pamoja, huku familia zisizo na uwezo, inakuwa vigumu kupata huduma, hasa kwa mzazi aliyejifungua.
Hali ilikuwa hivyo pia katika majengo mengine, likiwemo lile la watoto, ambako wagonjwa walionekana kuwa ni wengi kuliko wauguzi, kwani wakati kwa wastani muuguzi mmoja anapaswa kuhudumia wagonjwa kati ya 5-8, hapo muuguzi mmoja alijikuta akihudumia hadi wagonjwa 60.
Hata duka la dawa lililo chini ya hospitali hiyo, nalo lilionekana kama urembo tu, kwani kila aliyeandikiwa, alilazimika kutoka nje kwenye maduka binafsi.
Mmoja ya wagonjwa wakiwa hospitalini hapo. 
Katika wodi ya Mwaisela ambayo ina wagonjwa mseto wakiwemo wa vinywa, uvimbe, ajali za moto na kadhalika, ukosefu wa dawa ulileta tishio kubwa, hasa kwa mlipuko wa magonjwa ya kuambukizwa.
Kwa wagonjwa waliotakiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi, waliambiwa kurejea majumbani hadi hapo watakapoitwa kwa simu baada ya serikali kupata fedha.
Huduma ya maji pia ni tatizo lingine linalowakabili wagonjwa waliopo hospitalini hapo, kwani kwa wasiokuwa na uwezo wa kununua maji ya chupa, inawawia vigumu kuyapata kutoka Dawasco.
Vinginevyo wanapaswa kuyatumia yanayotoka katika kisima kilichopo hospitalini hapo, ambacho hata hivyo maji yake yanaelezwa kuwa na chumvi.
Wagonjwa wakinamama wakiwa katika moja ya wodi za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika chumba cha kuhifadhia maiti, uchunguzi umebaini hali ni mbaya zaidi, kwani wafiwa hulazimika kwenda kununua wenyewe dawa kwa ajili ya kuwahifadhi maiti wao. Pia ndani ya chumba hicho, zipo maiti za muda mrefu zinazohusu Chuo cha Kitabibu cha IMTU ambazo zimehifadhiwa hapo na hivyo baadhi ya watu kuomba serikali kuruhusu kuteketezwa kwa miili hiyo.
Afisa uhusiano mkuu wa Hospitali hiyo, Emaniel Eligalesha alisema matatizo yote yanayohusu  hospitali hiyo yatashughulikiwa muda mfupi ujao.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dkt. Seif  rashid akifafanua jambo.
Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Cosmas Mwaifwani alisema kutokana na deni kubwa la serikali, inakuwa vigumu kwao kukomboa kontena za dawa zilizokwama bandarini Dar es Salaam. “Hili tatizo la serikali kudai kodi kwa dawa zinazotolewa na wafadhili kutoka nje kunawakatisha tamaa, kwani kuna dawa zingine hazifai kutozwa kodi zikiwemo zile za waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi zikiwemo Kondom, hali hii inaweza kuwafanya wafadhili wasitishe kutoa misaada mbalimbali kwa vile ile inayotolewa haiwafikii wananchi kwa wakati,” alisema Mwaifwani na kuwafanya wagonjwa wengi kuondoka kwa vilio.