Wednesday, December 17, 2014

LOWASSA AWA GUMZO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima juzi, umemuibua na kumfanya waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa (pichani) kuwa gumzo kubwa, baada ya kutajwa na wagombea kuwa ndiye turufu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaani mrithi muafaka wa Rais Jakaya Kikwete.
Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Wagombea mbalimbali  wa CCM waliozungumza na gazeti hili baada ya uchaguzi huo juzi, walisema Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli, Arusha ndiye mtu pekee anayeweza kukabiliana na wapinzani, hasa wanaounda kundi la Ukawa, kwa kuwa vyama hivyo vina nguvu kubwa katika ukanda wa Kaskazini.
“Ukawa watakuwa na nguvu sana Kanda ya Kaskazini kutokana na Chadema, sasa kama CCM itamsimamisha mgombea anayekubalika kanda hiyo, ni wazi kuwa sehemu zingine za nchi itakuwa rahisi tu, Lowassa anakubalika sana Kaskazini, nadhani hata ndani ya chama chetu wenyewe wanajua,” alisema mgombea wa Uenyekiti wa mtaa mmoja uliopo Madale, wilayani  Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mgombea mwingine kutoka Sombetini jijini Arusha ambaye naye hakutaka kutajwa jina lake, alisema viongozi wengi wanaogombea katika vitongoji na vijiji, ni wafuasi wa Lowassa na wanaamini ndiye mkombozi wa chama tawala katika uchaguzi mkuu ujao, vinginevyo watapata taabu kushinda kwa vile watu wengi wanaotajwa kuwania nafasi hiyo wanapwaya ukiangalia sifa zao.
Naye Maalim Hassan Yahya Hussein aliyejiunga na CCM wiki iliyopita akitokea Chadema akiwa Mtaa wa Mzimuni , Magomeni  Dar, siku ya kupiga kura alikuwa na haya ya kusema:
“Kati ya watu wanaotajwa kuwania hii nafasi, nadhani mwenye kustahili ni yeye (Lowassa) tu kwa sababu hawa wengine itakuwa ni kazi sana kuwauza ndani ya chama, hawauziki, lakini Lowassa kila mtu anajua utendaji wake, anauzika na hata vijana wengi wanamkubali.”
Uchaguzi wa serikali za mitaa ulifanyika Jumapili iliyopita huku maeneo mengi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi wakipita bila kupingwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile vyama vya upinzani kukosa wagombea wenye sifa baada ya kuwekewa pingamizi.