Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyamisisi, Kata ya Kukirango, wilayani Butiama, Ryakora Kurwijira (34) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia shati lake akiwa ukweni baada ya kukataliwa na mkewe aliyekuwa akiishi naye.
Habari zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa karibu, zinaeleza kwamba marehemu alikuwa akiishi na mkewe aitwaye Doy Nyanyara katika Kijiji cha Nyatwari wilayani Bunda kwa kipindi cha miaka miwili, lakini ghafla mwanamke huyo alimfukuza marehemu kutoka nyumbani na kumwambia kuwa amepata mume mwingine wa kuishi naye, hivyo hamhitaji tena. Wawili hao walikuwa wakiishi nyumba ya mwanamke.
“Alipokaguliwa baada ya polisi kufika alikutwa na ujumbe unaosema: “Nimejinyonga kwa ajili ya kupenda,” kilisema chanzo hicho.
Imedaiwa kuwa baada ya mwanaume huyo kujinyonga, wazazi wa mwanamke huyo walitokomea kusikojulikana, ambapo mwili wa marehemu ulichukuliwa na polisi na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Bariadi kabla ya mwanamke huyo kuwapigia simu ndugu wa marehemu na kuwaambia kuwa ndugu yao amejinyonga.
Ndugu hao walifuatilia mwili huo na kuukuta katika hospitali hiyo na kuuchukua kwenda kwao Kiabakari ambako mazishi yalifanyika Desemba 19 mwaka huu.
Afisa mmoja wa polisi wa Bariadi ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa siyo msemaji alithibitisha kutokea kwa tukio hilo
Afisa mmoja wa polisi wa Bariadi ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa siyo msemaji alithibitisha kutokea kwa tukio hilo