Sunday, December 28, 2014

WATU 15 WAPOTEZA MAISHA WAKIWA NDANI YA MGODI HARAMU

Watu wasiopungua 15 wamepoteza maisha wakiwa ndani ya mgodi haramu huko kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Meya wa mji wa Kolwezi Deoda Kapenda amesema watu hao walipoteza maisha Ijumaa wakiwa ndani ya mgodi wenye kina cha fiti 20. Mji wa Kolwezi uko katika mkoa wenye utajiri wa madini wa Katanga.

Idadi kubwa ya wachimba migodi haramu huweka maisha yao hatarini wakijaribu kuchimba madini katika eneo hilo la mashariki mwa DRC. Mwezi Agosti mwaka 2012 zaidi ya watu 60 walifariki dunia katika mdogi huko Pangoy Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Pamoja na kuwa nchi hiyo ina utajiri mkubwa sana wa madini lakini idadi kubwa ya watu wake wanaishi katika umasikini mkubwa. DRC inakadiriwa kuwa na utajiri wa madini yenye thamani ya dola trilioni 24. Mashirika ya nchi za Ulaya na Marekani yanalaumiwa kupora utajiri wa madini katika nchi hiyo kubwa ya Afrika na hivyo kuwaacha watu wake wakiwa katika umasikini wa kupindukia.