Wednesday, January 14, 2015

BONGO MOVIES KWELI MMEKUBALI KUZIDIWA NA BONGO FLEVA?

 
LEO nimewakumbuka kwa mara nyingine ndugu zangu wasanii ambao mnafanya sinema za Kibongo, Bongo Movies. Sina haja ya kuwataja majina maana mko wengi, naweza nikamaliza barua yangu yote nikisema niwataje majina yenu mmojammoja. 
Bila shaka mu-wazima wa afya na wale ambao kwa namna moja au nyingine afya haiko poa, nawaombea kwa Mungu mpone haraka na mrudi katika hali ya kawaida, muendelee na kazi zenu za kujitafutia riziki.
 Mkitaka kujua hali yangu, binafsi nashukuru Mungu niko vizuri naendelea na mishemishe zangu kama kawaida.
Madhumuni ya barua hii ni kutaka kuwakumbusha ndugu zangu juu ya umuhimu wa nyinyi kuvuka mipaka.

 Hivi mnakumbuka kuna kipindi tasnia ya filamu ilikuwa juu kuliko Bongo Fleva? Ilikuwa ina mvuto mitaani kuliko kitu kingine. Watu walikuwa wakitaka kufuatilia habari zenu kuliko habari nyingine zozote katika jamii. 
Mnakumbuka mlianza kuvuka mipaka ya Tanzania kuliko tasnia nyingine. Kutokana na mvuto wenu, mliweza kufanya ziara mbalimbali katika nchi kama Uganda, Rwanda, Kongo na kwingineko ambako niwe mkweli, mlikubalika sana kuliko hata hapa nyumbani.

 Nguli wa sinema Vincent Kigosi ‘Ray’ na baadhi ya wasanii najua watakuwa ni mashahidi wazuri katika hili nilisemalo.
  
Ray anakumbuka jinsi alivyokuwa akiambatana na marehemu Steven Kanumba katika nchi mbalimbali, anajua mapokezi waliyokuwa wakiyapata kila walipokatiza katika nchi ambazo baadhi yao hazijui hata lugha ya Kiswahili.
 Vurugu zote hizo kwa sasa hatuzioni. Nakumbuka enzi hizo hata katika suala la umaarufu, msanii wa filamu alikuwa ni maarufu zaidi kuliko msanii wa muziki. Sijui nini kimetokea hadi mkawa kimya. Kanumba alithubutu na kuifanya tasnia ya simema ing’ae katika anga za Kimataifa.
 Aliweza kuvuka mipaka na kuwaleta wasanii wa Nigeria kuja kufanya kazi Tanzania, kweli kazi zikatoka na majibu yakaonekana.
 Ndugu zangu nini kinawashinda? Nini kimesababisha mkubali kuachwa na wasanii wa Bongo Fleva? Tunawaona wao tu sasa hivi ‘wakitusua’ na kufanya kazi na wasanii wa kimataifa, kwani nyinyi hampendi?
 Hamna wivu wa maendeleo? Mnakubali Diamond (Nasibu Abdul) peke yake aitangaze Tanzania.
 Mbona uwezo mnao? Kwa nini mkubali kuwa chini kila siku? Mimi naamini, ndani ya Bongo Movies, wapo wasanii ambao wana uwezo wa kuuvaa uhusika kuliko hata wa kimataifa ambao tunawafahamu. Kinachotakiwa ni kujiamini.
 Kama kipindi kile tuliona Kanumba na kina Ray wameweza, kwa nini msiweze sasa?
 Amkeni. Jitihada za mtu mmojammoja zinatakiwa, kila mtu ajitume kwelikweli ili kuhakikisha tunavuka mipaka ya Tanzania. Akifanikiwa mmoja au wawili heshima itakuwepo.
 Tunapenda kuona tasnia ya filamu inafanya vizuri sambamba na ile ya Bongo Fleva. Tujivunie muziki, tujivunie filamu na hata vipaji vingine ambavyo tunavyo Tanzania