MSIKIE kiungo wa Yanga, Andrey Coutinho, anachosema kwamba anafurahishwa na mfumo wa sasa wa timu yao chini ya kocha Hans Van Der Pluijm kwani unamfanya aonekane bora uwanjani tofauti na alipokuwa chini ya Mbrazili mwenzake, Marcio Maximo.
Coutinho aliliambia Mwanaspoti kuwa soka la kuzuia wakati wa Maximo lilikuwa linampa tabu na hakuufurahia mfumo huo tofauti na sasa ambapo amepewa uhuru wa kucheza kwa kushambulia.
Alisema hakuwa na amani wakati Yanga ilipokuwa chini ya Maximo kwani alikuwa anajua safari ya kurudi kwao Brazil inaweza kumkuta muda wowote kwa kuwa angeonekana wa kawaida uwanjani kama ilivyokuwa kwa Genilson Santos ‘Jaja’ ambaye pia aliponzwa na mfumo wa kuzuia.
“Sikuwahi kufurahia soka wakati nipo na Maximo hapa Yanga, kwani tulikuwa tunacheza kwa kuzuia na sikupata muda mwingi wa kushambulia kwa uhuru na kazi ilikuwa kubwa ya kushuka kuzuia na wakati huohuo mpandishe mashambulizi,” alisema.
Chanzo:Mwanaspoti