Tuesday, January 20, 2015

GODBLESS LEMA NA MWENZAKE WAWAAHIDI WANANCHI KUMTOA BUNGENI KWA NGUVU PROF MUHONGO

Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless
Lema amesema atamtoa kwa mabavu bungeni
Waziri wa nishati na madini,Profesa Sospetre
Muhongo katika kikao kijacho cha Bunge endapo
atakuwa hajaondolewa kwenye nafasi hiyo.
Mkakati huo wa Lema umeungwa mkono na
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema),
Joshua Nassari ambaye pia amepanga kumtoa
bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge.
“Keshokutwa nakwenda bungeni kufanya kazi
moja tu, nikimkuta Muhongo bungeni ndipo
nitafukuzwa ubunge moja kwa moja,” alisema
Lema huku akishangiliwa wananchi na kuongeza;
“Nikimkuta Muhongo bungeni na Chenge bado ni
viongozi mimi nitakwenda kumshika Muhongo
nimtoe bungeni kwa sababu Katiba inaruhusu kila
raia kukemea uovu.”
Profesa Muhongo na Chenge ni miongoni mwa
viongozi ambao Bunge liliazimia wawajibishwe na
mamlaka zao kutokana na kashfa ya uchotwaji
mamilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Hata hivyo, wakati Rais Jakaya Kikwete
akilihutubia Taifa, Desemba 22 mwaka jana
kupitia wazee wa Dar es Salaam, alitangaza
kumweka kiporo Profesa Muhongo kwa siku mbili
au tatu, ahadi ambayo haijatekelezwa.
Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema anayehusishwa na sakata hilo
alishatangaza kujiuzulu na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka akifutwa kazi.