Tuesday, January 6, 2015

MBINU MPYA ZA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA


 Baadhi ya wanawake wa Kitanzania waliofungwa katika magereza ya China na Hong Kong, walishika ujauzito kama moja ya mbinu ya kupitisha dawa za kulevya bila kugundulika kwenye viwanja vya ndege na mipaka mingine ya kimataifa. Mwananchi limebaini.
Watanzania wanne walio katika magereza ya China na Hong Kong walijifungua watoto kwa nyakati tofauti wakiwa wanatumikia vifungo na wamekiri kuwa walibeba ujauzito kama mbinu ya kupitisha dawa hizo bila kukaguliwa.
Watoto wanaozaliwa magereza baada ya kufikisha mwaka mmoja hupelekwa katika vituo vya watoto yatima na kusomeshwa na Serikali ya China hadi pale wazazi wao watakapomaliza adhabu.
Imebainika kuwa watoto wawili wapo katika vituo hivyo, mmoja tayari yupo Tanzania baada ya bibi yake kumrejesha na mwingine bado yupo gerezani na mama yake.
Wanawake hao ambao wote wana umri wa kati ya miaka 20 na 30 walieleza masikitiko yao jinsi ambavyo wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wanavyowarubuni ili kubeba dawa hizo kwa ahadi za kuwapa fedha nyingi.
“Tunapata mimba makusudi kwa sababu tulijua kuwa katika viwanja vya ndege vingi wajawazito hawakaguliwi hasa wakiwa na mimba kwa hiyo tungebeba unga na kuupeleka China, halafu baadaye tungerudi nchini na kutoa mimba au tukiamua tunajifungua,” alisema mmoja wa wafungwa hao.
Hata hivyo, mbinu hiyo ilifanikiwa katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lakini haikufua dafu katika viwanja vya ndege vya China, Hong Kong, Macau na Guang Zhou.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athuman alisema hana taarifa za Watanzania hao lakini ofisi yake inafanya taratibu za kuwasiliana na China ili kujua hali za wanawake hao.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki alisema kwa kawaida kila mtu hukaguliwa kwa uangalifu bila kujali mjamzito au la. Akielezea namna wanavyopimwa, Malaki alisema kwanza kila msafiri hupimwa kwa mashine ya kawaida ambayo hubaini uwepo wa kifaa chochote kisichotakiwa mwilini kwa mfano chuma kama hereni, bangili, mikanda lakini si ndani ya tumbo.
“Iwapo mashine ya awali itatoa mlio hata baada ya msafiri kutoa vitu vya chuma, basi atatakiwa kwenda katika chumba maalumu cha ukaguzi wa mikono,” alisema.
Kamanda wa kitengo cha Polisi cha Dawa za Kulevya, (SACP), Godfrey Nzowa alisema wapo wanawake kadhaa raia wa Zambia, Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini na Malawi ambao wamefungwa katika magereza ya Tanzania kwa kusafirisha dawa za kulevya wakitumia mbinu hiyo ya ubebaji wa mimba.
Alisema mbinu hizo zinatumiwa na wanawake kwa sababu wajawazito hawakaguliwi kwa mashine za x-ray na kwamba wengi walikamatwa kutokana na taarifa za kikachero.“Hata magereza ya hapa tunao na wamejifungua watoto wakiwa gerezani, lakini wajue kabisa kuwa watakwepa mashine lakini taarifa zinatusaidia na ndiyo maana nasema taarifa ni nguvu,” alisema.
Pamoja na kukamatwa kwa raia wa kigeni wanaotumia mbinu hiyo, Kamishna Nzowa hakuwa na taarifa za Watanzania waliokamatwa nje ya nchi kwa kutumia mbinu hiyo.
Septemba mwaka jana, raia wa Canada, Tabitha Ritchie alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Columbia kwa kubeba dawa za kulevya kwenye mimba ya bandia, mbinu ambayo ilibainika baada ya kuhojiwa na maofisa wa uhamiaji kuhusu umri wa mimba yake na walipomgusa tumboni walibaini kuwa tumbo lilikuwa baridi na gumu.
Askari mmoja wa Kitengo cha Dawa za Kulevya wa JNIA, (jina linahifadhiwa), alieleza wazi kuwa hakuna mashine ya kujua mtu aliyemeza dawa hizo zaidi ya kuhisi tu kwa mbinu za kiaskari.
Alisema mara nyingi watu waliomeza dawa hizo hukamatwa kwa kuhisiwa na baada ya kupekuliwa huamriwa kuruka kichura au kujisaidia ili kujua iwapo wana ‘mzigo’ tumboni.
Hata hivyo, askari huyo alisema kwa kawaida wajawazito hawawezi kurushwa kichura au kulazimishwa wajisaidie kutokana na hali zao.
Miongoni mwa wanawake waliobeba mimba kwa ajili ya kubeba dawa za kulevya na wasichana maarufu nchini, mmoja wao mtoto wake sasa analelewa katika kituo cha watoto yatima China.
Baada ya kupata taarifa hizo, Mwananchi ilizitafuta familia za wafungwa hao ambazo hazikuwa na taarifa kuwa na ndugu zao walikuwa na ujauzito walipokuwa wakisafiri.
Baadhi ya waliohojiwa walisema walipata taarifa za ndugu zao kuwa na watoto wachanga lakini hawakuwa na habari za ujauzito.
“Hata hivyo, ninamshukuru Mungu kwa kuwa amepata mtoto na anaendelea vizuri, kutokana na uwezo wetu kuwa mdogo siwezi kwenda kumchukua mjukuu wangu huko Hong Kong, mwache akae kituoni hadi mama yake atakapoachiwa,” alisema mama wa mmoja wa wafungwa hao.