Tunasikitishwa na kuongezeka kwa matukio ya milipuko ya mabomu yanayotengenezwa kienyeji katika sehemu mbalimbali hapa nchini, kiasi cha wananchi wengi kujaa hofu kutokana na madhara ambayo yamesababishwa na mabomu hayo tangu matukio hayo yalipotokea kwa mara ya kwanza hapa nchini Oktoba 2002 katika jiji la Arusha. Katika jiji hilo pekee, yalitokea matukio saba ya aina hiyo tangu Oktoba 2002 hadi Septemba mwaka jana.
Hakuna asiyejua kwamba matukio hayo yalisababisha vifo na kujeruhi idadi kubwa ya watu, mbali na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na kujenga hofu kwa wananchi. Tulishuhudia jinsi matukio hayo yalivyotishia uchumi wa nchi yetu kutokana na kukwamisha shughuli za kitalii. Sisi tulipaza sauti kulaani vitendo hivyo vya kigaidi na kuitaka Serikali kuchukua hatua siyo tu kwa kudhibiti vitendo hivyo, bali pia kuwakamata wahusika wa vitendo hivyo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Pamoja na matukio hayo kwa kiasi fulani kudhibitiwa na vyombo vya dola jijini Arusha, matukio kama hayo sasa yamehamia mjini Songea mkoani Ruvuma ambako kati ya Septemba na Desemba mwaka jana, yalitokea matukio matatu mfululizo ya kutupa mabomu yaliyotengenezwa kienyeji. Tofauti na matukio ya mabomu ya jijini Arusha, matukio ya Songea yaliwalenga askari wa usalama barabarani na wengine waliokuwa katika doria kwa nyakati tofauti. Katika tukio la tatu lililotokea siku 10 zilizopita, mtu mmoja alifariki dunia baada ya kulipukiwa na bomu wakati akijiandaa kulitupa kuelekea kwa polisi wa kikosi cha usalama barabarani.
Wakati wananchi wakiendelea kujadili tukio hilo la mjini Songea, wiki iliyopita bomu lililotengenezwa kienyeji, likafungwa katika kifurushi na kupelekwa nyumbani kwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Iramba mkoani Singida, Bi Halima Mpita kama zawadi ya Krismasi, lililipuka na kuacha maswali mengi ambayo hadi sasa Serikali imeshindwa kuyatolea ufafanuzi wa kuridhisha. Matukio ya mabomu hayo yaliwahi pia kutokea katika baadhi ya mikoa, ikiwamo Kigoma, Kagera na Mara.
Tumeorodhesha matukio hayo yote siyo tu kuonyesha ukubwa wa tatizo, bali pia kujenga hoja kwamba pengine kuna siri iliyofichika nyuma ya milipuko hiyo. Inatuwia vigumu kuelewa jinsi matukio hayo yanavyoweza kuachwa kuendelea kutokea nchini. Kama tulivyodokeza hapo juu, hali hiyo imeacha maswali mengi kuliko majibu kutokana na Serikali kushindwa kutegua kitendawili kuhusu watu wanaohusika na milipuko hiyo. Kwa maneno mengine, vyombo vya ulinzi na usalama vimeshindwa kutafuta mbinu za kutokomeza vitendo hivyo, ikiwa ni pamoja na kuwakamata wote wanaohusika, ingawa Jeshi la Polisi limekuwa likitoa kauli na ahadi ambazo haizitekelezi. Haiingii akilini kuona vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinashindwa kuwakamata wahalifu hao, ambao wanaonekana kujiimarisha sehemu mbalimbali nchini.
Sisi tunasema uhalifu huu kamwe haukubaliki. Serikali lazima itambue kwamba bila kutafuta kiini na chanzo cha vitendo hivyo kila vinapotokea haitaweza kuvitokomeza, badala yake itabaki kuwa nyuma ya matokeo kama tunavyoshuhudia hivi sasa. Katika kupambana na uhalifu, ingekuwa vyema pia kama Serikali itaondoa mazingira yanayosababisha kuzaliwa kwa vikundi vya uhalifu kama ‘Panya Road’. Ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya vichocheo vinavyozalisha vikundi hivyo na tusishangae kama wengi wa watengenezaji wa mabomu ya kienyeji ni vijana waliozagaa mitaani kwa kukosa ajira.