Thursday, January 29, 2015

NIMEFANIKIWA KUIPATA HOTUBA YA LIPUMBA ALIYOTAKIWA KUISOMA WAKATI WA MAANDAMANO.....INASEMA WANAWAKE WALIBAKWA NA WATU KUUAWA NA POLISI


Siku ya leo siyo siku ya furaha hata kidogo na wala si siku ya kujifaharisha, ni siku ya kihistoria kwa chama chetu, ni siku ya kukumbukwa sana.
  Miaka kumi na nne iliyopita tarehe kama ya leo tarehe 27 Januari, 2001 na tarehe kama ya jana tarehe 26 Januari 2001, Wanachama wenzetu waliojitoa muhanga, leo hii hawapo wamekwenda mbele ya haki katika siku kama hii, mama zetu na dada zetu wanaikumbuka kwa huzuni kubwa siku kama hii ya leo, kwani si vyema kuwakumbusha lakini inatubidi tuyakumbuke yaliyowakuta siku kama hii ya leo.
  Mama zetu na dada zetu walibakwa na kunajisiwa na askari wa kidhalimu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, na wengine wakaachwa mayatima kwa waume zao kuuwawa na askari hao hao wa kidhalimu, na kutuachia mayatima na wengine hadi leo wanaishi na ulemavu.

Kwa mara ya kwanza nchi yetu ilizalisha wakimbizi kwa ndugu zetu na wanachama wenzetu ilibidi wakimbilie Mombasa nchini Kenya katika kunusuru maisha yao, wapo wengine waliyakimbia makazi yao na kuishi maporini na wengine walifia baharini wakati wakijaribu kujinusuru.

Tukizikumbuka nasaha nzuri alizozitoa Mwenyekiti wetu Prof. Ibrahim Haruna Lipumba mwezi Oktoba 2001 pale Bwawani Hotel Zanzibar wakati wa kutiliana saini mkataba wa Muafaka alisema kwamba “Ni vyema tukaendelea kuyakumbuka yaliyotokea ili ibaki kuwa kovu itakayotufanya tusiweze kuyarudia tena yale yaliyosababisha maafa kama yale kutokea”. 
  Tukiikumbuka siku kama ya leo inatubidi pia kuzikumbuka siku mbili kabla ya leo, yaani Januri 25, 2001 wakati Mwenyekiti Prof. Ibrahim Haruna Lipumba alipopigwa na wenzake na kuvunjwa mkono na askari wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi na kumkamata pamoja na Viongozi wengine waandamizi na wanachama wenzetu na kuwafungulia kesi ya uchochezi.

Mwenyekiti alikuwa akitekeleza misingi ya Demokrasia kwa mujibu wa katiba ya nchi ya kukusanyika na kutoa mawazo yako hadharani, jambo ambalo aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Wiliam Benjamin Mkapa alishatoa amri kwenyae hotuba yake ya kuuaga mwaka 2000 na kuingia mwaka mpya wa 2001 kwa kukataza mikutano ya hadhara pamoja na maandamano akidai kwamba uchaguzi umemalizika na washindi wameshajulikana hivyo ni vyema tukaungana katika kuijenga nchi kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi.
  Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba katika hotuba yake pale Mbagala Zakiem kabla ya kukamatwa kwake, pamoja na kusisitiza nchi kuendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala bora, demokrasia na utawala wa sheria, lakini pia aliahidi kuwa kwa vile nchi yetu imepoteza sifa na dira ya kuitwa nchi yenye misingi hiyo, suluhisho pekee ni kufanya maandamano nchi nzima na yeye ndie atakae yaongoza maandamano hayo ambayo aliyatangaza kufanyika siku ya tatu yake yaani tarehe 27, Januari 2001.

Katika maandamano hayo tulikuwa na madai manne;
  1. Kutomtambua Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na kutaka uchaguzi urudiwe
  2. Kudai Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
  3. Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
  4. Katiba Mpya
Pamoja na Mwenyekiti wetu kumkamata wakidhani kwamba watakuwa wamefanikiwa kutuzuia tusiandamane, halikadhalika watu wawili waliuliwa siku moja kabla, yaani tarehe 26 Januari pale Zanzibar, kwa agizo la aliekuwa Makamo wa Rais Marehemu Dk. Omari Alli Juma wakiamini watakuwa wametutisha kiasi cha kutosha, lakini wapi, tuliandamana na wenzetu wengine wakawa muhanga. MWENYEZI MUNGU ZILAZE ROHO ZA MAREHEMU WOTE WALIOJITOA MUHANGA MAHALI PEMA PEPONI – AMINY!!

Narudia tena kwa msisitizo; ni hali ya kusikitisha kila inapofika siku kama ya leo, inatukumbusha madhila tuliofanyiwa ndani ya nchi yetu kwa kudai haki, inatukumbusha damu ya ndugu zetu iliyomwagika kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha ulemavu walioupata ndugu zetu kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha dada zetu na mama zetu walioachwa vizuka kwa waume zao waliuwawa kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha binti, dada zetu na mama zetu walibakwa kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha watoto walioachwa yatima kwa sababu yakudai haki, inatukumbusha watu walisamehe Ubunge wao na Uwakilishi wao katika baraza la wawakilishi kwa sababu ya kudai haki.

Muhanga huu waliojiotoa ndugu zetu, ndio matokeo na mafanikio yaliyojitokeza sasa hivi hadi kufikia wengine kujidai na kujifaragua na kufikia hata kutoa kejeli na maneno ya kifedhuli na kebehi, wakati ndugu zetu wanapoteza maisha yao kwa kuandamana wao waliona tunaigiza.

Mafanikio katika madai yetu yale manne;
  1. Kuhusu kutomtambua aliekuwa Rais wa Zanzibar Amani Karume na kudai uchaguzi kurudiwa; kulipelekea kufikiwa kwa muafaka kati yake na Katibu Mkuu wetu Maalim Seif Sharif Hamad, ndio uliopelekea kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ambapo chama chetu kipo varandani Ikulu kwa Maalim Seif kuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, na tunatarajia mwishoni mwaka huu Oktoba 2015 tunaichukua wenyewe Ikulu ya Zanzibar.
  2. Kuhusu madai ya Tume Huru ya Uchaguzi, kwa upande wa Zanzibar Tume hiyo iliundwa pamoja na kugubikwa na wingi wa makada wa Chama cha Mapinduzi kutokana na mfumo mbovu wa uteuzi, lakini tunaamini huu ni mwanzo tu, kilichobakia ni kupigania maboresho ya Tume hiyo kuwa Huru Kwelikweli na si kama ilivyo sasa. Tunaiasa CCM na Serikali yake Bila Uchaguzi huru na wa Haki Oktoba 2015 Taifa linaweza likarudia historia ya mwaka 2001.
  3. Kuhusu Daftari la Kudumu la Wapiga kura tulifanikiwa kulipata, nalo huwa linachafuliwa na wajanja wa Chama cha Mapinduzi kwa kulitia mikono, lakini nalo tutalipigania kuhakikisha linatumika ipasavyo na kama tulivyokusudia wakati wakulidai, na kwa vile kuna maboresho ya mfumo mpya wa daftari, tunawaomba wanachama wetu tuhamasishane tujitokeze wote kwenda kujiandikisha kwa Dar es Salaam uandikishaji unaanza Februari 15 mwezi ujao.
  4. Kuhusu kupatikana kwa Katiba Mpya, ambapo ndani yake kungekuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na mengineyo yaliyomuhimu kwetu sisi katika kuleta haki na usawa kwa wote, CCM na Serikali yake wameuteka mchakato huo hatua za Mwisho za Bunge la Katiba na kuyatupilia mabali mambo yote muhimu yatokanayo na michango ya wananchi wenyewe yaliyokusanywa na Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuingiza mambo yao yenye maslahi ya kifisadi kwa Taifa. CUF – Chama Wananchi tunatoa AGIZO ni marufuku kwa wanachama na wapenzi wetu wote nchi nzima kujitokeza kwenda kupiga kura ya maoni, kwani kushiriki kwa aina yoyote hata kupiga kura ya hapana ni kubariki mchakato haramu uliofanywa na Mafisadi wa Chama cha Mapinduzi.
Waheshimiwa Wanachama katika kuyaenzi Maadhimisho haya tunatakiwa kuongeza nguvu, mshikamano, umoja na kupeana nafasi kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea kwa kuzingatia katiba yetu na kanuni zetu, kwa kuhakikisha kwamba chaguzi zijazo za kura za maoni ndani ya chama zinatupatia Wagombea wanaokubalika katika jamii katika nafasi za Udiwani, Ubunge na Urais.
 
 Tuepuke majungu na makundi yanayoleta faraka ya wenyewe kwa wenyewe, kama waliowengi wanakuona huwezi kuwafikisha wanakotaka, wewe kubali yaishe, ikifika wakati wa kuaminika kwako watakupa nafasi, tuache kususa na hata kuingia msituni baada ya matokeo ya kura za maoni ndani ya chama.

Waheshimiwa wanachama wenzetu, tunawaomba na tunawasihi sana tuyatumie maadhimisho haya katika kushauriana namna bora ya kuboresha chama chetu, na hasa katika kuongeza wanachama watakao kipatia chama chetu ushindi, na tunaendelea kusisitiza kimbilio letu kubwa liwe ni kwa vijana wetu tulionao.
  Ni aibu kubwa sana kama utakuwa na kijana mwenye umri wa kupiga kura na asikuunge mkono wewe kama mzazi wake au mlezi wake, tukumbuke wosia wa Muasisi wetu Marehemu Shaaban Khamis Mloo, kuwa tuhamasishane kunzia katika sahani ya chakula, kitandani, ndani ya shuka, uwani, barazani, chumba kwa chumba, mlango kwa mlango, nyumba kwa nyumba, katika vijiwe vya kahawa, mabaraza ya bao, kinamama wanaposukana, vilabu vya mipira, maofisini na kila penye mkusanyiko wa watu na tujiwekee ahadi kila mwanachama mmoja imalizikapo miezi mitatu angalau awe ameingiza ndani ya chama sio chini ya wanachama wapya watatu.

MWISHO;
Tunawaomba radhi na tunawapa pole Wanachama wenzetu wote wa CUF – Chama cha Wananchi, kwa kuwakumbusha siku hii nzito kwetu na ya majonzi makubwa TUNAJUA MMEGUSWA, lakini tujifute machozi yetu kwa kuenzi moyo wa kujitoa kwa ajili ya chama ili kuhakikisha haki inapatikana na chama chetu kinapata ushindi katika uchaguzi huu ujao, hii ndio namna bora ya kuwaenzi WAHANGA wetu, tukumbuke “WOGA NI ADUI WA HAKI”


HAKI SAWA KWA WOTE Prof.Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti CUF Taifa