Askari wawili wa Jeshi la Polisi katika Kituo cha Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani, wameuawa baada ya kushambuliwa kwa silaha na majambazi, waliovamia kituo hicho na kuiba silaha baada ya kufanikisha mauaji.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi liko katika msako mkali, huku Mkuu wa jeshi hilo, IGP, Ernest Mangu akitangaza donge nono la Sh milioni 20 kwa watakaofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo na silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, Ikwiriri, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema majambazi hao walitumia silaha kuwaua askari hao.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 8 usiku katika kituo hicho cha Polisi cha Ikwiriri. Aliwataja askari waliokufa kuwa ni mwenye namba E 8732 Koplo Edgar Milinga na WP 5558 Konstebo Judith Timothy.
Alisema licha ya kufanya mauaji hayo, pia majambazi hayo yalipora silaha tano za moto aina mbalimbali, zikiwemo SMG 2, SAR 3 na risasi 60. Pia, walichukua mabomu mawili ya machozi.
Kamanda alisema kuwa pia watu hao, waliharibu kwa kulipiga risasi gari la Polisi la kituo hicho lenye namba za usajili PT 1965.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema tukio hilo la kusikitisha, halitapita hivi hivi, bali jeshi limeelekeza nguvu zake huko kuhakikisha wahusika wanakamatwa.
Alisema tayari Mkuu wa Jeshi ametangaza dau la Sh milioni 20. Pia, alisema katika kuongeza kasi ya msako, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja akiwa na timu ya makachero, yuko eneo la tukio kuhakikisha wahusika, kokote waliko, wanasakwa na kutiwa mbaroni.
“Hili ni sawa na tukio la kigaidi, Jeshi la Polisi litakabiliana na wahusika kokote waliko, lazima wakamatwe. Kikubwa tunaomba ushirikiano wa wananchi, tunaamini wengi ni raia wema na watalisaidia jeshi kufanikisha jukumu hilo la kukomesha uhalifu nchini,” alisema Advera.
Aliwataka wananchi kuelewa Jeshi la Polisi liko imara, hivyo wasiwe na hofu yoyote juu ya tukio hilo. Alisisitiza kuwa wahusika wote watadhibitiwa na kushikishwa adabu