Thursday, January 8, 2015

WADAIWA KUWAUA WANAWAKE BAADA YA KUFANYA NAO MAPENZI


Wafanyabiashara Abubakar Kasanga (28) na Ezekiel Kaseregela (25), wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi mbili tofauti za mauaji ya kukusudia ya wanawake waliokuwa wakifanya nao mapenzi.
Inadaiwa kuwa Kasanga na Kaseregela walikuwa wakiwarubuni wanawake kadhaa, kufanya nao mapenzi na kutumia mwanya huo kuwalewesha dawa, kuwaibia na kuwaua.
Akiwasomea shtaka la mauaji katika kesi PI namba 1, Wakili wa Serikali, Janeth Kitali alidai kuwa Novemba 14, 2014, Kasanga aliyekuwa akiishi nyumba ya wageni na Kaseregela akiishi Tandika, walimuua kwa makusudi Jacqueline Masanja.
Baada ya kusomewa shtaka hilo linalowakabili, Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawaruhusiwi kuongea chochote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kulisikiliza shtaka hilo isipokuwa Mahakama Kuu.