Saturday, January 17, 2015

WAPINZANI WASEMA WATAHAKIKISHA WANAFUNZI WALIOFUKUZWA UDOM WANAREJESHWA


KAMBI rasmi ya upinzani bungeni imesema itawasaidia kwenye masuala ya kisheria wanafunzi waliofukuzwa kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kutokana na kuandamana kudai kupewa fedha za kujikimu.
 
Akizungumza juzi katika ofisi za Bunge, Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo alisema kuwa tatizo hilo linatokana na serikali kutokuwa na mipango ya kuhakikisha maslahi ya wanafunzi hao yanatekelezwa.
 
Alisema watawasaidia masuala ya kisheria kuhakikisha wanarejeshwa chuoni kwani walichokifanya ni haki na kusema hawezekani wanafunzi wakakaa chuoni kwa miezi mitatu bila kupewa fedha za kujikimu.
 
Juzi uongozi wa chuo hicho uliwaachisha masomo wanafunzi watatu vinara wa maandamano hayo ya wanafunzi wa programu maalum ya walimu wa sayansi.
 
Mmoja wao alifukuzwa moja kwa moja na wawili wana nafasi ya kujieleza kuhusika kwao na maandamano hayo yaliyochafua hali ya hewa na kusababisha wanafunzi 84 kutiwa mbaroni.
 
Walioondolewa shuleni ni Kyambwene Msatu(Rais wa serikali ya wanafunzi), Philip Mwakibinga (Waziri Mkuu) na Ismail Chande (Katibu Mkuu).
 
Naye, Naibu Waziri Kivuli Elimu, Joshua Nasari alisema endapo wanafunzi hao watafukuzwa basi atawaongoza wanafunzi hao hadi kwa Waziri Mkuu kudai haki zao.