Shule za sekondari zilizopo katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara ambazo baadhi ya viongozi wa serikali walisoma, ziko mbioni kufungwa kutokana na ukosefu wa chakula baada ya wazabuni kusitisha huduma.
Wazabuni hao wamesitisha kutoa ya chakula kwa shule hizo kutokana na kuidai serikali zaidi ya Sh. milioni 400.
Baadhi ya viongozi wa serikali waliowahi kusoma katika shule hizo ni pamoja na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Shule hizo ambazo zimetangazwa rasmi kufungwa ifikapo Febuari 8, mwaka huu ni Sekondari ya Wavulana Ndanda ambayo Rais Mstaafu Mkapa alisoma na Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi ambayo Spika Makinda alisoma.
Nyingine ni Shule ya Sekondari Ndwika Shule ya Sekondari ya Wavulana Chidya.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jana kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo, Juma Bushiri, alisema hatua ya kutaka kuzifunga shule hizo inatokana na wazabuni kusitisha huduma ya kusambaza chakula kwa kuwa wanaidai serikali kiasi hicho cha fedha.
Alisema kuwa tatizo hilo linasabishwa na Serikali Kuu kushindwa kuleta fedha za kutosha za huduma ya chakula kwa shule hizo.
Alifafanua kuwa fedha kikikotolewa kila mwanafunzi anapaswa kupewa Sh. 1,500 kwa siku, kiasi ambacho hakikidhi mahitaji kulingana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Bushiri alisema fedha hizo kidogo zinazotolewa na serikali, ndiko kulikosababisha deni kufikia kiasi hicho kikubwa.