MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa klabu ya Real Madrid na Timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, ambaye kwa sasa ni Mwanasoka bora duniani kufuatia kunyakua tuzo ya FIFA Ballon D’or amesema kuwa bado yupo kwenye mazungumzo mazuri na kocha wake wa zamani, Sir Alex Ferguson.
Ronaldo alipohojiwa na Shaffih Dauda, mwandishi mahiri wa habari za michezo nchini kupitia mtandao wake wake wa Shaffihdauda.com na Dauda TV, moja kwa moja akiwa Zurich, Uswisi, alisema kuwa anawasiliana na Sir. Ferguson ambaye alimfundisha alipokuwa Uingereza akitumikia klabu ya Manchester United na kudai kuwa kocha huyo anamuita ni mchezaji bora.
“Ninazungumza mara nyingi na Sir Alex Ferguson na tuna mawasiliano mazuri, ananishauri vizuri, ni jambo zuri, bado ninamkumbuka, mara nyingi ananiambia mimi ni Bora” Alisema Ronaldo.
Akizungumzia matarajio yake ya hapo badaye juu ya kutetea Ubingwa huo baada ya kuwapiga chini wapinzani wake Lionel Messi na kipa Manuel Neuer, Ronaldo alisema anatarajia mwakani kurejea Uswisi kutetea Ubingwa.
“Kila kitu kinawezekana, inategemea ni kitu gani umefanya kwa mwaka mzima, Lakini kushinda tuzo kama hii inaongeza chachu kwangu binafsi tutaona nini kitatokea kwa mara nyingine” Amesema .
Dauda kwa utafiti wake amegundua kuwa Mashabiki wengi wa Manchester United walikuwa wanamsapoti Ronaldo hadi kunyakua kikombe hicho na alipotaka kujua kama yeye anatambua hilo, Ronaldo alisema kuwa anatambua.
“Ni kawaida kwasababu nilikuwa na wakati mzuri nilipokuwa Manchester United na ndio ilikuwa mwanzo wangu wa mafanikio ndio maana mashabiki wananiunga mkono” Ameongezea Ronaldo.
Ronaldo hakusita kusema kuwa hasimu wake Lionel Messi anampa changamoto kutokana na kiwango chake, kitu ambacho kinapelekea Mreno huyo pia kufanya vizuri akijituma ili aweze kuwa zaidi ya Muargentina huyo.
“Inawezekana ni kweli, kufanya kwake vizuri inanipa hamasa mimi kufanya vizuri muda wote, inawezekana ikawa sababu ya mimi kufanya vizuri pamoja na timu yangu” Amesema Nyota huyo wa Kireno.
Bingwa huyo wa FIFA Ballon D’or mara tatu, ametoboa siri ya yeye kufanya vyema muda wote ambapo ametoa funzo kwa wachezaji wa Kitanzania kujituma na kufanya mazoezi sana tena kwa muda mrefu wa ziada.
“Kwa mwaka mzima muda mwingi mimi nafanya kazi, ni mwendelezo mzuri katika kazi yangu na nimetwaa tuzo nyingi binafsi, mazoezi ndio siri ya mimi kufanya vizuri na usishangae kuniona hapa tena” Ameongezea Ronaldo ambaye siku anachukua Ubingwa huo kesho yake yeye ndio alikuwa wa kwanza kufika mazoezini.
Kwa kumalizia mazungumzo, Ronaldo alizungumzia kutokuwepo kwa marehemu baba yake mzazi ambapo amesema kuwa inampa changamoto kubwa na kupigana kusaka mafanikio.
“Yeye ndio sababu mimi niko hapa, kimwili hatupo naye lakini kiroho tupo naye, ananiangalia na kunipa nguvu za kufanya mafanikio. Ni sehemu ya Maisha yangu na ni mtu muhimu sana katika maisha yangu, siwezi kuzungumzia zaidi” Amemalizia Ronaldo.