Monday, February 9, 2015

BABA APIGWA PINGU KWA KUMTESA MTOTO

Hekaheka! Baba mkubwa aliyetajwa kwa jina la Mohamed Said a.k.a Muddy, mkazi wa Tegeta-Msufini jijini Dar amepigwa pingu akituhumiwa kumfanyia ukatili wa kutisha wa kumsulubu mtoto wa kiume wa mdogo wake, mwenye umri wa miaka sita (jina linahifadhiwa).
Baba mkubwa aliyetajwa kwa jina la Mohamed Said a.k.a Muddy akiwa amepigwa pingu kwa madai ya kumtesa mtoto wa mdogo wake.
Tukio hilo kusikitisha lilijiri Februari 6, mwaka huu maeneo hayo ambapo awali inadaiwa kuwa Muddy alimchukua mtoto huyo kutoka kwa wazazi wake wanaoishi mkoani Mtwara kwa lengo la kuja naye Dar kwa ajili ya kumsomesha.
DOZI YA VIPIGO
Ilidaiwa kwamba, kinyume na lengo hilo, jamaa huyo alipomfikisha Dar alianza kumfanyia ukatili wa dozi ya vipigo.
Mama mzazi wa mtoto huyo(kushoto) akilia kwa uchungu.
KILIO CHA MAJIRANI
Wakizungumza na Ijumaa Wikienda juu ya tukio hilo, majirani walisema kuwa jamaa huyo amekuwa akimshushia kipigo mtoto huyo mara kwa mara kwa kutumia mti wa ufagio, bomba la plastiki na waya wa umeme huku adhabu kama kumnyanyua miguu juu kichwa chini, kumnyanyua juu kwa kumshika masikio na kushinda muda mrefu bila kula vikiwa ni sehemu ya maisha ya mtoto huyo.
TAARIFA KWA MJUMBE
Majirani hao walidai kuwa walichoshwa na vitendo hivyo na kila walipomkataza Muddy, waliambulia vitisho jambo lililowafanya watoe taarifa kwa Mjumbe wa Shina, Maulid Mheza ambaye aliahidi kulifanyia kazi.
Sehemu ya majeraha mguuni aliyopata mtoto huyo baada ya kuteswa.
SIKU YA TUKIO
Habari zilidai kwamba, siku ya tukio, majira ya asubuhi, Muddy alimwangushia mtoto huyo kipigo kilichomsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili hadi akaishiwa nguvu.
Ilidaiwa kwamba majirani walipoona hali ya hatari, walitoa taarifa kwa mjumbe wao ambaye alifika nyumbani kwa Muddy akiwa na polisi kutoka Kituo cha Wazo Hill.
MTOTO APUMUA
Wakiwa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo walimkuta mtoto huyo akiwa hoi hivyo alipowaona alipumua na kumshukuru mjumbe kwa kufika huku akiwaonesha mahali alipo baba yake ambapo alikuwa akioga bafuni.
Msamaria mwema akiwa na mtoto huyo.
MTUHUMIWA ATOKA KWA MBINDE
Muddy alipoamriwa na polisi atoke bafuni, alitoa lugha chafu jambo lililowafanya askari hao kutumia nguvu kwa kupiga risasi tatu hewani na nguvu za watu watano ndizo zilizofanikisha kumpandisha kwenye karandinga kwa kuwa alikuwa na nguvu za ajabu.
MWENYEWE AJITETEA
Katika utetezi wake, Muddy alisema kuwa alikuwa akimpiga mtoto huyo kwa kuwa hakuwa akielewa wakati alipomfundisha kusoma.
Mjumbe wa Shina, Maulid Mheza akimbeba mtoto huyo.
MJUMBE ATAHARUKI
Akizungumza na waandishi wetu, Mjumbe Mheza alisema kuwa hali aliyomkuta nayo mtoto huyo ilimshtua kwani alikuwa hawezi kutembea wala kuzungumza vizuri kutokana na woga huku mwili wake ukiwa umevimba na kujaa makovu yaliyotokana na vipigo kutoka kwa baba yake huyo.
MTOTO AJAZA UMATI POLISI
Katika hali ya kushangaza kila mtu aliyesikia habari za mtoto huyo alifika kituo cha polisi kujionea kwa macho yake hali iliyowalazimu polisi kuwatawanya kutokana na kuongezeka kwa idadi yao.
RB aliyokatiwa mtuhumiwa kwa shambulio la kudhuru mwili.
VILIO
Naye mama mtu aliyekuwa ametua Dar alipopigiwa simu na mjumbe alifika kituoni hapo na kuungana na wanawake wengine kuangua vilio baada ya kumuona mwanaye akiwa katika hali mbaya kiafya.
Hadi Ijumaa Wikienda linaanua jamvi kituoni hapo, mtuhumiwa alikuwa akishikiliwa na polisi kwa jalada la kesi namba WH/RB/1101/2015 -SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI huku mtoto huyo akikabidhiwa kwa mama yake ambaye alipewa fomu ya matibabu P-F3 kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya kiafya.