Tuesday, February 10, 2015

CHADEMA: HATUTAKUBALI KURA ZETU ZIIBIWE TENA.....MBOWE AZINDUA MAFUNZO YA VIJANA 200 WA RED BRIGADE NA WACHEZA KARETI


Chama  Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimejipanga kuhakikisha katika uchaguzi Mkuu hawaibiwi kura.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freemon Mbowe  wakati akizindua mafunzo ya Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha chama hicho (Red Brigade), kwa vijana 200 wa  Kanda ya Kati pamoja na Kikosi maalum cha Karate.

“Katika  uchaguzi huu hatutaki  kulalamika tena kwamba tumeibiwa kura na tutahakikisha  tutaomba  kura kwa wananchi na tutazilinda,” alisema Mbowe.

Alisema endapo watakubali kuibiwa kura maana yake hawapo tayari kuongoza.

Mbowe aliwataka  vijana hao wa Brigade kutokukilinda chama peke yake bali pia kiwe chachu ya ulinzi kwa jamii inayowazunguka kwenye maeneo yao.

Alibainisha kuwa Chadema  kitaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi kwa vijana nchi nzima.

"Vijana  hawa lazima wajenge moyo wa kujitolea, chama kilijengwa na watu wenye moyo huo ambao baadhi walipata madhara mbalimbali ikiwamo kupoteza maisha,” alisema Mbowe.

Alisema wajenge sifa ya kuwa wakombozi wa Taifa na  malipo mengine siyo lazima walipwe hapa duniani bali  watapata  kwa Mungu.

Awali akisoma risala kwa niaba ya kikosi hicho, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Anatoly Isidory, alisema kikosi hicho kinachojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, kina jumla ya vijana 4,271.

Alisema kati ya hao, 200 wamepewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kulinda chama na mali zake, viongozi pamoja na kura katika Uchaguzi Mkuu.

“Hadi sasa yapo mafanikio mengi ambayo tumeyapata, ikiwamo kulinda mikutano ya chama pamoja na kuwalinda viongozi wetu katika mikutano hiyo,” alisema Isidory.