Inadaiwa kuwa kimenuka kati ya msanii Rehema Chalamila ‘Ray C’ na baba mwenye nyumba wake, Hussein Kassim baada ya mdada huyo kudaiwa kugoma kutoa vyombo vyake kwenye mgahawa aliopangishwa na mkataba kuisha.
Msanii Rehema Chalamila ‘Ray C’.
Ray C aliyekuwa akitoa huduma ya chakula na vinywaji kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar kupitia mgahawa wake maarufu kwa jina la Ray C Restaurant, alifikia hatua hiyo baada ya kudai kuwa na yeye alipwe fidia ya shilingi laki moja kwa ajili ya ukarabati alioufanya.
Akizungumza baba mwenye nyumba hiyo alisema baada ya Ray C kugoma kutoa vitu vyake, aliamua kwenda kumshtaki kwa mabosi wao wa kitengo cha Methadone ambacho kinamtibu Ray C na yeye mwenyewe kwani wote ni waathirika wa madawa ya kulevya.
Baba mwenye nyumba huyo alidai baada ya kumshtaki katika kitengo hicho, Ray C aliahidi kwenda kuvunja ukuta ambao aliujenga na kuchukua vitu vyake hivyo baada ya siku mbili na angepeleka ufunguo kwa mkuu wa kitengo cha Methadone.
Baba mwenye nyumba wa Ray C.
“Mkataba uliisha Januari 19, mwaka huu lakini akakaa kimya mpaka nilivyoenda kumwambia maana alikuwa ameshikilia ufunguo wangu huku mimi nimeshapata mteja mwingine.
“Kila nikimwambia aje kutoa vitu vyake anakataa na kusema mpaka nimlipe laki moja aliyofanyia ukarabati wakati mimi hakunishirikisha, sikutaka kufika huku maana Ray C ni mwenzangu tunakunywa naye dawa lakini ukorofi wake ndiyo umesababisha haya yote,” alisema Hussein.
Baada ya siku mbili kupita, mkuu wao alimtaka aende kisheria ambapo alienda kuripoti katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Minazini, Mwananyamala na Ray C akaandikiwa barua ya wito mara ya kwanza, hakwenda baada ya hapo akaandikiwa kwa mara ya pili, Jumanne iliyopita ambayo alifika akiwa amechelewa.
Ray C baada ya kuambiwa dhumuni la wito huo kwa afisa mtendaji, aliahidi kutoa vitu hivyo siku iliyofuata.Alipoulizwa Ray C kuhusiana na tukio hilo, alikiri kupelekwa serikali ya mtaa na kusema vitu vingi vinavyoongelewa dhidi yake havina ukweli.
“Hayo wanayozungumza ni mambo ya Kiswahili tu, mimi nimeshaachia fremu ila bado kuchukua vitu vyangu tu, nenda serikali ya mtaa utapata maelezo kamili maana hao wanataka kunichafulia jina tu,” alisema Ray C.