HATIMAYE kuvamiwa kwa vituo vya polisi na kuporwa silaha huku askari wake wakiuawa kikatili kumejulikana kunafanywa na nani kufuatia gazeti hili kunasa mkanda wa video wa mtu mmoja anayejiita Kaisi Bin Abdullah akijitapa kufanya hivyo kwa lengo la kukusanya silaha ili kulipa kisasi siku si nyingi!
Ijumaa liliunasa mkanda huo kutoka kwa mtu mmoja aliyekataa kujitambulisha kwa jina wala kusema anakotokea hapa nchini huku akisema: “Una maneno ya hatari sana, naogopa kujianika, nitauawa.”
Kaisi Bin Abdullah akiwa amejiziba sura.
“Siwezi kutaja jina wala mahali ninapoishi, sitaki kupigwa picha, kama hamtaki niwapatie taarifa hii acheni niondoke,” alisema mtu huyo huku akinyanyuka kitini jambo lililowafanya wakuu wa dawati kukubaliana na matakwa yake na kuendelea na mahojiano.
Baadaye ilipatikana fursa ya kuuangalia mkanda huo; Bin Abdullah ametumia dakika 11: 03 kuzungumzia mambo mbalimbali lakini kubwa kuliko yote ni kuliponda Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuwakamata wenzao katika imani na harakati (zinazohifadhiwa kwa sasa) na kuwashikilia kwenye mahabusu mbalimbali nchini.
ALIANZA KWA KUSEMA
Bin Abullah ambaye kwenye mkanda huo amevaa nguo nyeusi kama ninja na miwani ya giza, alizungumza kwa kirefu, akitoa wito lakini mbele akasema:
“Tumeshaungana ili kupambana. Mkoa wa Mtwara zaidi ya wenzetu kumi na saba walikamatwa kwa makosa ya dhuluma, makosa ya kupanga, makosa ya ugaidi. Ishirini na moja wamekamatwa Zanzibar wako katika Gereza la Segerea (Dar). Wenzetu wengine kumi na nane wamekamatwa Mwanza wako katika Gereza la Kisongo, Arusha. Ndugu zangu, wenzetu wengine kumi na saba wameuawa Mtwara kwa amri ya ...(anamtaja waziri).”
ADAI WAMECHOKA NA SUBIRA
“Subira yetu imefika mwisho na tulichokuwa tunasubiri Mungu ameshatupa. Tunatoa ahadi kilichopo hivi sasa tunatoboa jahazi wote tuzame.”
WENZAO WAACHIWE HURU
“Tunatoa rai, wenzetu waliopo Gereza la Kisongo waachiwe huru. Hapa hatumtishi mtu yeyote yule.”
KUHUSU VITUO VYA POLISI
“Pili, agizo la Ernest Mangu IGP, umetangaza uliwenguni kwamba umewakamata wote waliovamia vituo vya polisi na umezikamata silaha zote. Ukweli ni kwamba unatetea tumbo lako. Hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa na wala silaha hazijakamatwa.
“Mungu ametukubali. Katika Kituo cha Polisi Ushirombo (Kilimanjaro) tumeweza kuvamia kituo, tukaweza kutoa roho za polisi na tukaweza kuchukua silaha, tunazo.“Tumevamia Kituo cha Polisi Ikwiriri (Pwani), tumeweza kuchukua silaha za kutosha, tumeweza kuchukua mabomu ya kutosha. Tunazo silaha tunasubiri muda zianze kufanya kazi.
“Ernest Mangu nakupa changamogto, hivi sasa tuna uwezo...(maneno yanahifadhiwa kwa usalama) wakati wowote ambao tunataka.”
HAKUNA UPINZANI?
“Tumeweza kuchukua silaha bila kuwa na silaha yoyote. Ndugu zetu wa Tanga wameweza kuchukua silaha wakiwa hawana silaha yoyote. Ikwiriri tumechukua silaha tukiwa hatuna silaha yoyote, mpaka sasa tumeshachukua roho tano za polisi.”
VITISHO VYA JUMLA
“Ndugu zangu, ...mlikuwa mkinisubiri nitoe tamko, natoa kauli rasmi...” alihitimisha Abdullah, huku vitisho vya jumla kwenye tamko lake vikiwahusu polisi, viongozi wa ngazi za juu serikalini pamoja na mikusanyiko ya ibada.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu.
TAMKO NGUNGURI LA IGP
Baada ya video hiyo, Ijumaa lilimuibukia Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu na kuzungumza naye kuhusu mtu huyo na kumkabidhi video ambapo alisema:
“Nawashukuru sana kwa kuleta video hii, huu ndiyo ushirikiano unaotakiwa, nawaomba wananchi video za aina hii wazikatae kwa sababu ni kosa kuwa nazo na watu kadhaa wameshakamatwa kwa kuwa nazo.
“Sisi kama jeshi la polisi tunajua kuwa kuna watu wanadhani kufanya uhalifu kama huo kutawasaidia kutimiza matakwa yao, lakini ukweli ni kwamba polisi wapo imara na nina uhakika watuhumiwa watakamatwa kwa kushirikiana na raia wema.”
SHEHE MKUU AMKANA
Baada ya kuzungumza na IGP, Ijumaa lilimtafuta Shehe Mkuu Tanzania, Mufti Shaban Simba na kumsimulia kuhusu kuibuka kwa Bin Abullah na kutaka kujua pengine anamfahamu.
“Kwanza hizo taarifa hizo ndiyo nazisikia kutoka kwako. Hilo jina ulilonitajia (Bin Abdullah) sijawahi kulisikia labda muangalie kwa wenzetu upande wa pili.”
KUMBUKUMBU ZA NYUMA
Katika gazeti ndugu na hili, Uwazi, Toleo la Januari 28 mpaka Februari 2, mwaka huu ukurasa wake wa mbele kulikuwa na habari yenye kichwa; KUUAWA KWA POLISI IKWIRIRI; MAZITO YAIBUKA!
Katika habari hiyo, Uwazi lilichimba kwa kina kuhusu kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi Ikwiriri na kuuawa kwa askari wake wawili, Edger Jerald Mlinga (43) na Judith Timothy (32).
Watu hao waliodhaniwa ni majambazi walifanikiwa kupora bunduki 7, risasi 60 na mabomu kadhaa yaliyokuwa ndani ya kituo na kukimbia bila kukamatwa.
Baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi kwenye eneo la tukio walisema wana wasiwasi watu hao si majambazi bali ni kundi la kigaidi ambalo lina mkakati wa kukusanya silaha kwa ajili ya matumizi batili siku za baadaye, jambo ambalo limeanza kujionesha kupitia video iliyonaswa na Gazeti na Ijumaa.
KUTOKA DAWATI LA IJUMAA
Tunawaomba wananchi kwa ujumla kutokuwapa nafasi watu wa aina ya Abdullah wanaoeneza chuki kwa lengo la kuwagawa watu na kuleta machafuko, badala yake kila anayeashiria shari ni vema taarifa zake zikafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili amani ya taifa iendelee kudumu.
Aidha, tunalitaka jeshi la polisi pamoja na vyombo vya usalama kulichukulia kwa uzito tamko la mtu huyo anayedai kuwa ni kiongozi wa ugaidi, kumsaka na kumtia hatiani pamoja na wafuasi wake wote.