Saturday, February 7, 2015

NINGEKUWA MIMI GODBLESS LEMA, NINGETHIBITISHA KAULI YANGU KUHUSU CHAGONJA

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Jonathan Lema.
Kwako Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Jonathan Lema. Najua hunijui na hakuna mazingira yanayoweza kutukutanisha pamoja lakini hilo halinizuii kukufikishia ujumbe ninaotaka kukupa.
Mheshimiwa, mimi sikuzaliwa Oktoba 26, 1976 kama wewe. Sikusoma Shule ya Msingi Kalangala kuanzia mwaka 1983 hadi 1989 wala sikujiunga na Sekondari ya Geita na baadaye kusoma kidato cha tano na sita kwenye Shule ya Sekondari ya Kolila kama wewe.
Mimi sisomi Chuo cha Cambridge unakochukua stashahada kama wewe. Nasisitiza mimi si mbunge wa Arusha mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo kama wewe, mimi ni mlalahoi tu, nang’aza sharubu mjini.
Hata hivyo, ningekuwa mimi katika nafasi yako, nakuhakikishia ningetoa ushahidi hadharani kuhusu madai mazito uliyomtolea Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, Paul Chagonja kwamba anahusika katika kupanga mkakati wa kutekeleza vitendo vya utekaji wa vituo vya polisi nchini na kupora silaha.
Ndiyo! Nisingeacha kauli nzito kama hii, ipite tu kama upepo huku watu wengi wakibaki na sintofahamu kwamba ulikuwa unakijua unachokisema au ndiyo propaganda za kisiasa.
Sijui uhusiano uliopo kati ya Chagonja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu mpaka wewe useme kwamba Chagonja anaratibu vitendo hivyo kwa nia ya kumhujumu Mangu ili kuchafua taswira ya uongozi wake mbele ya macho ya jamii.
Wengi walitegemea kuwa baada ya kutoa kauli hiyo bungeni wakati ukichangia mjadala kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, ungekuja na ushahidi wa kuipa nguvu hoja yako nzito uliyoitoa.
Kama ulikuwa hujui, kauli uliyoitoa imewashangaza wengi na hivi sasa kila mmoja ana shauku ya kutaka kujua mchele ni upi na chuya ni zipi, watu wanautaka ukweli mheshimiwa.
Kama ulizungumza kisiasa, basi ni vyema ukaueleza umma wa Watanzania kwamba ulichokisema hakikuwa na ukweli wowote lakini kama una ukweli wa hoja hiyo, watu wanasubiri kwa hamu kujua kwa kina hizo njama zinazofanywa na Chagonja.
Watu wamechoka kunyanyaswa na jeshi la polisi, wanataka kufahamu hao wanaotoa mamlaka ya watu kupigwa na kujeruhiwa, wao wana ukamilifu wa kiasi gani.
Kujua udhaifu wa mtu anayekunyanyasa ni hatua kubwa kuelekea kwenye kukomesha unyanyasaji unaofanyiwa, watu wengi wanataka kufahamu udhaifu wa viongozi wa juu wa jeshi la polisi, ndiyo maana kauli yako imepokelewa tofauti kabisa na kauli nyingine ulizowahi kuzitoa.
Ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, ningetoa ushahidi wa nilichokisema ili watu waniamini. Wasalaam.