“Masikio hayawezi kuvuka kichwa, kiongozi wa serikali usiyetaka kuambiwa ukweli na chama nenda kalale, acha kazi.” Hii ni kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye aliyoitoa wakati akikemea ule aliouita uzembe wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Nape na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana bado wanaendelea kupaza sauti kuwa baadhi ya wateule wa mwenyekiti wao wa chama, Jakaya Kikwete hawaendani na kasi ya kutumikia jamii.Mwaka jana waliibuka na kibwagizo kuwa, serikali yao inayoongozwa na Rais Kikwete ina rundo la mawaziri mizigo, utashi wao ukawa ni kumtaka mwenyekiti awatimue wasikigharimu chama.
Wakati kionjo hicho cha mawaziri mizigo kikionekana kupoa, wameibua kingine kinachoitwa waziri mzururaji; wakimaanisha Nyalandu. Wametoa hoja ang’olewe akalale kwa kuwa ameonesha kuishindwa nafasi ya uwaziri.
Wamesema wazi kuwa, masikio hayazidi kichwa, tafsiri ni kwamba wanaoingoza serikali ni masikio ya CCM ambacho ndiyo kichwa cha rais hadi katibu tawala. Hapa ndipo ninapoitafakari CCM na serikali yake kiasi cha kuchanganyikiwa.
Kwa nini? Nape na Kinana wanaposema karibu kila walikopita wamekutana na migogoro ya ardhi ikiwahusisha wananchi, hifadhi za taifa na kwa upande mwingine wawekezaji na waziri yupoyupo tu; anazurura, kuna kitu cha kutafakari.
Najiuliza; Kinana anapomuona mzururaji Rais Kikwete aliyemchagua katika nafasi hiyo ya uwaziri anakuwa wapi, kalala? Nape anapomuona Nyalandu kuwa ameshindwa kutekeleza jukumu lake; Rais Kikwete, kasafiri? Nachanganyikiwa kabisa!
Ukifuatilia ziara za Nape na Kinana zinazoitwa za kujenga chama kila walipopita viongozi hao hotuba zao nyingi zimejaa ukosoaji kwa baadhi ya watendaji wa serikali, kwa vinywa vyao wamekiri hadharani kuwa udhaifu huo unakidhoofisha chama chao.
Jambo la kujiuliza; hivi kichwa (CCM) na masikio (watendaji) havina ushirikiano ndiyo maana jamii inashuhudia mkanganyiko huo wa kimtazamo? Ikiwa viungo hivi havishirikiani katika utendaji, wananchi wanavigawanyaje ili kinachoonekana dhaifu wakichukie?
Tangu lini mchongoma ukazaa machungwa? Kamwe chemchemi ya maji haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu. Naomba nisikilizwe hoja zangu kwa makini.CCM ya Nape na Kinana, mwenyekiti wake ni Rais Kikwete ambaye ni mkuu wa uteuzi wa karibu nafasi zote nyeti za nchi hii, nafasi hizohizo ndizo zinazopigiwa kelele na wasafisha chama kuwa ni dhaifu ki-utendaji!
Kwa nini tusifike mbali zaidi ya fikra hizo, tuvuke mipaka ya ufahamu mpaka tuusogelee ukweli kuwa anayewaangusha siyo Nyalandu na uzururaji wake bali aliyemteua ambaye ni mwenyekiti wa CCM.
Nashangaa kuaminishwa kuwa chama kinaweza kuwa mtetezi wa wanyonge kwa kiwango wanachoonesha akina Kinana, kuipita serikali ambayo inaongozwa na mwenyekiti wa Kinana.
Nashangaa kuaminishwa kuwa chama kinaweza kuwa mtetezi wa wanyonge kwa kiwango wanachoonesha akina Kinana, kuipita serikali ambayo inaongozwa na mwenyekiti wa Kinana.
Hivi mashauriano ya chama kifanye nini hawa akina Nape wanayafanyia nyumbani kwao au ofisini? Wanajipangia watakavyo au vikao vya chama na ridhaa ya viongozi wa ngazi za juu akiwemo mwenyeti ndiyo vinavyotoa baraka ya ziara na kupokea mrejesho wa kilichofanywa na watumwaji!
Ikiwa chama kinaongozwa kwa mfumo, iweje rais ambaye ni mwenyekiti asijue kuwa, Nyalandu ni mzururaji na kumtimua kazi mara moja! Waliitwa mawaziri mizigo wakaendelea kudunda kwenye nafasi zao; Nyalandu kaambiwa aache kazi lakini bado anapanda ndege na kulipwa mshahara unaotokana na kodi za wananchi.
Naomba Nape awaambie wananchi wafanye nini ili watenganishe kichwa na masikio kwa sababu wamechoshwa na umaskini. Asipofanya hivyo ipo siku wataamua kukata shingo, wakiondoe kichwa pamoja na masikio yake kisha wavitupe jalalani! Nachochea tu.