MSANII wa muziki Bongo, Khadija Maige ‘Kadja Nito’ amenaswa na Mapaparazi wetu akiingia nyumbani kwa sangoma aliyefahamika kwa jina la Kimweri aliyewahi kuripotiwa kumng’arisha msanii mwenzake Menina Attick ‘Menina Ladiva’ kisanaa.
Msanii wa muziki Bongo, Khadija Maige ‘Kadja Nito’ akiwasili kwa sangoma huyo.
Chanzo chetu cha kuaminika kilichopo jirani na eneo hilo kilieleza kuwa kimekuwa kikimshuhudia msanii huyo akifika mahara hapo kufuata matibabu huku dhumuni likiwa ni kusaka umaarufu ili awe staa mkubwa wa muziki kama walivyo wasanii wengine wenye majina makubwa Bongo.
“Kuna yule msanii alitamba na kibao chake cha Maumivu, mara kwa mara huwa anafika kwa huyu Dk. Kimweri muda wa jioni, nikifuatilia mazungumzo yao kikubwa anachomlalamikia mganga wake huwa ni kusaka usupastaa na jana nilimsikia akisema anaweza kufika leo jioni,” alisema sosi huyo.
Baada ya kupata taarifa hizo mapaparazi wetu walitinga eneo hilo na kuweka kambi jirani na nyumba ya mtaalamu huyo na kukaa zaidi ya saa moja wakiangaza huku na huko, mishale ya saa kumi na mbili jioni ndipo msanii huyo alionekana akishuka kwenye Bajaj akiwa amevalia baibui na ushungi, kisha sangoma huyo akajitokeza kumpokea wakatokomea ndani bila kujua walipigwa picha.
Kutokana na ishu hiyo gazeti hili lilimtafuta Kadja, alipoulizwa alionyesha mshtuko na kukiri kufika kwa sangoma huyo ambaye alidai alikwenda kumsabahi kwa sababu wanafahamiana na si kufuata tiba.
Mtaalamu huyo alipovutiwa waya ili kutaka kujua lengo la msanii huyo kufika ofisini kwake alijibu kwa kifupi: Nashindwa kukizungumzia hicho mnachohitaji sababu siruhusiwi kutoa siri za wateja wangu.”