Wednesday, April 1, 2015

KIBA: NJOONI MUONE JINSI NINAVYOPIGA NA ‘LIVE’ BENDI

Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Saleh ‘Kiba’.
Said Ally, Dar es Salaam
MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Saleh ‘Kiba’, ametamka wazi kuwa, amejipanga vya kutosha kuhakikisha anawapagawisha mashabiki wake watakaojitokeza katika shoo ya Mwana Dar Live ambayo itaunguruma katika Sikukuu ya Pasaka, Aprili 5, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kiba alisema amejipanga vya kutosha kuhakikisha anachengua akili za mashabiki wake ambao watajitokeza siku hiyo ya shoo ambapo kwa mara ya kwanza ataimba wimbo wake wa Chekecha Cheketua ‘live’.
“Nimejipanga vya kutosha kuhakikisha ninatoa burudani nzuri ambayo itampagawisha kila shabiki ambaye atajitokeza ukumbini hapo, tena siku hiyo wala hakutakuwa na kuimba kwa kutumia CD ‘playback’, mambo yote nitayafanya kwa kutumia ‘live’ bendi na nimeshafanya maandalizi ya kutosha kuvitumia vyombo hivyo,” alisema Kiba.
Mbali ya Ali Kiba, pia katika shoo hiyo ya Mwana Dar Live watakuwepo pia wasanii Isha Mashauzi ‘Jike la Simba’ pamoja na bendi yake ya Mashauzi Classic ambao wanatamba na nyimbo kama Mapenzi Yamenivuruga,Tuacheni Tulale na mfalme wa nyimbo za vigodoro, Seleman Jabir ‘Msaga Sumu’ ambaye anatamba na nyimbo kadhaa zikiwemo Hunifao, Apangalo Mola na nyingine kibao.
Pia katika kutoa burudani kwa kila mtu, kundi zima la sarakasi la Masai Warriors, litakuwepo kuwapagawisha watoto wote watakaojitokeza ukumbini hapo kuanzia mida ya saa tano asubuhi hadi saa 12 jioni.