Wednesday, April 29, 2015

UKATILI ULIOJE! WAZAZI WAMPIGA, WAMFUNGA KAMBA MTOTO WAO, WAMFUNGIA NDANI

Na Dustan Shekidele
Katika hali inayoonyesha ukatili wa ajabu, mwanamke mmoja aliyejulikana  kwa jina la  Asha Mohamed, akishirikiana na mumewe, walimfunga kamba miguu na mikono mwanaye wa kumzaa Salum Mohamed (9) na kumfungia ndani ya nyumba yake huku wenyewe wakienda kusikojulikana muda mrefu Jumatatu iliyopita huko Mkundi, nje kidogo ya mji wa Morogoro.
Polisi wakimfungua kamba mtoto huyo alizokua amefungwa na wazazi wake.
Tukio hilo la kusikitisha lilifanyika ikiwa ni adhabu ya mtoto huyo kutokana kosa la kuchana chandarua kwa miguu, kitendo alichokifanya usiku wa Jumapili, ambako licha ya kupigwa kwa zaidi ya saa mbili mfululizo, pia alinyimwa chakula na hivyo kulala na njaa.
Polisi wakiwa wamembeba mtoto huyo.
Kwa mujibu wa majirani, Asha na mumewe ambaye ni baba wa kambo wa mtoto huyo, wamekuwa na tabia ya kumtesa, kitendo ambacho awali, kiliwahi kumfanya atoroke nyumbani hapo kukimbilia mjini kwa bibi yake, umbali wa zaidi ya kilomita kumi
Mama mzazi wa mtoto huyo aliefahamika kwa jina la Asha Mohamedi.
Kwa mujibu wa majirani Mwanamke huyo na mumewe kwa muda mrefu walikuwa wakimfanyia vitendo vya kikatili mtoto huyo”kuna wakati mtoto huyu aliamua kutembea kwa kwa miguu kutoka hapa mkundi mpaka mjini kwa bibi yake umbali wa kilomita 10.
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na mtoto huyo baada ya kufunguliwa kamba.
“Wazazi wake jana majira ya saa 3 mpaka saa 5 usiku walimpiga sana huyu mtoto, cha ajabu asubuhi walimfunga kamba na kumfungia kwa nje na kufuli kubwa na wenyewe kwenda kwenye shughuli zao, alishindwa kwenda shule, tulipomuuliza kupitia dirishani, alisema alipewa adhabu hiyo baada ya kuchana chandarua, kwa uchungu tukaamua kutoa taarifa kwako,” alisema Mage Luzimamu, mmoja wa majirani.
Baada ya mwandishi kupata taarifa hizo aliwasiliana na Jeshi la Polisi ambapo askari walienda hadi ilipo nyumba hiyo na kulazimika kuvunja mlango na baadaye kumfungua mtoto huyo na kuondoka naye. Mama mzazi alipatikana na kukiri kuhusika na tukio hilo, ambapo alijitetea kuwa alimfunga kamba kama sehemu ya adhabu na siyo mateso.
Mume wa mama huyo alikimbia baada ya kusikia taarifa za kusakwa kwake lakini Polisi wamesema watamtafuta hadi wamtie mbaroni.