Thursday, May 7, 2015

AIBU! KIBOSILE ANAYEFAHAMIKA KWA JINA LA MANGI PESA ANASWA LIVE UFISADI WA VYANDARUA


Ufisadi! Kibosile mmoja aliyefahamika kwa jina la Mangi Pesa amekamatwa na polisi akiwa na shehena ya vyandarua vya serikali vya msaada ambavyo hugawiwa bure, akivitoa kwenye mifuko yake na ‘kuvipaki’ kwenye mifuko ya vyandarua vinavyouzwa.

Tukio hilo la kushangaza lilijiri Jumamosi iliyopita kwenye ‘godauni’ la jamaa huyo lililopo katika nyumba moja iliyopo Sinza C jijini Dar kwa msaada wa taarifa kutoka kwa wasamaria wema waliochoshwa na ufisadi huo wa Mangi.

Habari zilieleza kuwa Jeshi la Polisi kwenye Kituo cha Kijitonyama almaarufu Mabatini jijini Dar lilipokea taarifa za kuwepo skendo hiyo ambapo lilifika eneo la tukio mara moja kama kawaida yake na kumdaka Mangi akiwa tumbo wazi ambapo walimng’ang’ania vilivyo baada ya kutaka kuleta ‘rabsha’.
Dakika sifuri baadaye, Timu ya Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers nayo ilifika eneo hilo na kumkuta Mangi akiwa chini ya ulinzi ambapo alipokaguliwa alikutwa na shehena hiyo ya vyandarua vya msaada.
Kwa mujibu wa wasamaria wema hao, jamaa huyo amekuwa akijihusisha na mchezo huo kwa muda mrefu huku ikisemekana kuwa huwa anakula dili na wahusika ambao ni vigogo serikalini wanaomuuzia kwa bei chee naye ‘kuvipaki’ upya na kwenda kuuza kwa bei ya juu.
Akiwa amezungukwa na shehena hiyo kwenye godauni lake huku mzigo mwingine ukiwa kwenye magari yaliyokuwa ndani ya uzio wa nyumba hiyo, Mangi alionekana kutaharuki kwani hakujua kama angenaswa katika mazingira hayo.
Hata hivyo, polisi hao walimtuliza na kumpiga pingu kisha kumbeba kwenye gari na vidhibiti vyake na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Mabatini kwa ajili ya upelelezi zaidi wa tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake.Habari zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni zilieleza kuwa Mangi aliachiwa kwa dhamana akisubiri kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.