Baadhi ya mastaa wa tasnia ya sinema za Kibongo wanaounda Klabu ya Bongo Movie, wamemliza laivu mlezi wao ambaye amekuwa akiwasapoti kwa hali na mali, Catherine Ambakisye ‘Mama Loraa’ baada ya kumuangushia bonge la pati la kushtukiza (suprise) ambalo hakulitarajia.
Wahusika hao walimfanyia Mama Loraa pati hiyo hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Baloko uliopo maeneo ya Vijana-Kinondoni jijini Dar ikiwa imeandaliwa na mastaa wa kike wa Bongo Movie.
Baadhi ya mastaa hao walioshuhudiwa na gazeti hili ni pamoja na Jennifer Kyaka ‘Odama’, Halima Yahya ‘Davina’, Sabrina Rupia ‘Cathy’, Salma Salmin ‘Sandra’, Herith Chumila na wengine, ikiwa ni kuthamini mchango wake mkubwa aliuofanya katika kukuza tasnia ya filamu Bongo.
Akizungumza huku akitokwa machozi, Mama Loraa alifunguka: “Sikuwa na mpango wowote wa kufanya kitu chochote lakini nimeshangazwa na maandalizi haya yaliyonitoa machozi ya furaha maana sikutarajia.”
Katika sherehe hiyo, walimwalika mumewe Loraa ambaye hakujua kuna shughuli ambapo alikabidhiwa zawadi ya ua kwa ajili ya siku yake hiyo.Wasanii hao walimpa Mama Loraa zawadi mbalimbali vikiwemo viatu, magauni na vitu vingine kisha watu wakaanza kunywa na kula hadi wakasaza.