Wednesday, May 20, 2015

DIAMOND 'AMAZING' SHOO YAKE ALIYOFANYA LONDON YAACHA GUMZO

Musa Mateja
AMAZING! Hiyo ndiyo kauli pekee unayoweza kuitamka kuakisi shoo baab’kubwa aliyoifanya mkali wa wimbo wa Nasema Nao, Nasibu Abdul ‘Diamond’, London, Uingereza, Risasi Mchanganyiko linakujuza zaidi.
Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond’ akipagawisha wakazi wa jiji la London.
Shoo hiyo iliyoacha gumzo la aina yake nchini humo kutokana na kupata idadi kubwa ya mashabiki, ilifanyika Jumapili iliyopita katika Ukumbi wa Royal Regency, maeneo ya Manor Park.
Chanzo chetu kilichoambatana na msafara wa Diamond kwenye shoo hiyo ijulikanayo kama Diamond are Forever, kiliweka bayana kuwa shoo hiyo ilikuwa ya kustaajabisha (amazing) kwani ilikadiriwa kuwa na watu zaidi ya 1500 ambao ni Wabongo waishio nchini humo waliochanganyika na wazungu.
Akitambulishwa mbele ya mashabiki.
“Jamaa kapiga shoo ya nguvu, watu walijaa kweli, si Wabongo pekee bali Wazungu nao walikuwepo. Si zile shoo za kupiga sebuleni ambazo wasanii wengi wa Kibongo huwa wanafanya. Yani hadi leo (Jumatatu) kila mtu anaizungumzia. Imeacha gumzo la aina yake.
“Ilikuwa yenye hadhi maana kiingilio kilikuwa ni shilingi laki moja na ishirini kwa V.I.P na elfu tisini viti vya kawaida, Wazungu walichanganyikiwa hadi ikabidi waulize Who is Diamond? (Diamond ni nani?) wakaambiwa na meneja wa msanii huyo, Babu Tale kuwa ni msanii anayeiwakilisha Tanzania akitokea Tandale, Dar es Salaam,” kilimwaga data chanzo hicho.
Mbali na umati huo ‘kuinjoi’ nyimbo za Diamond kama Kamwambie, Mbagala, Kesho na Nasema Nao na nyingine kibao, shoo hiyo iliongeza msisimko kufuatia uwepo wa balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Peter Kalaghe ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza machache jukwaani, burudani ikaendelea.