Na Haruni Sanchawa
Mke wa marehemu Kapteni John Komba, Salome Komba, amemtaja mrithi wa kiti cha Ubunge Jimbo la Mbinga Magharibi kuwa ni Cassian Njowoka. Akizungumza na gazeti hili, mama Komba alisema Njowoka ambaye ni Mkurugenzi wa Chuo cha Ualimu, Kibamba na Chuo cha Uuguzi Dar es Salaam alikuwa bega kwa bega na mumewe katika kuwaletea maendeleo.
“Ilikuwa marehemu akiwaza kusaidia kitu fulani kwa wapiga kura wake, Njowoka alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanachangiana kwa hali na mali kufanikisha jambo hilo kwa wananchi wa Mbinga Magharibi, hivyo anaona anastahili kumrithi,” alisema mama Komba.
Nao baadhi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Jimbo la Mbinga Magharibi, kwa nyakati tofauti wametaka Njowoka kuchukua fomu ya kugombea wakati ukiwadia kwani walidai ni kamanda wao wa (UVCCM) Wilaya ya Nyasa pia ni mlezi wa Umoja wa Wanawake Tanzania wilayani hapo.
Njowoka alipoulizwa na gazeti hili kama yupo tayari kugombe nafasi hiyo ya Komba, hakukanusha wala kukubali bali alikiri kupokea maombi hayo kutoka kwa wanachama wengi wa jimbo hilo.“Natafakari, muda ukiwadia nitaishirikisha familia na washauri wangu kuona kama niingie au la kwenye kinyang’anyiro hicho,” alisema Njowoka.