Monday, June 8, 2015

HUU NDIO UKWELI! KINACHOWAMALIZA MASTAA NI HIKI

Kullu nafsin zaikatul maut! Huo ni mstari katika kitabu kitakatifu cha Quran unaomaanisha kila nafsi itaonja mauti. Wimbi la vifo vya wasanii linazidi kuitingisha tasnia ya burudani Bongo.
Ndani ya kipindi kifupi cha miaka michache iliyopita, tumeshuhudia wasanii wengi wa filamu na muziki, maarufu na wasio maarufu, wakipoteza maisha kwa sababu mbalimbali.


Marehemu Recho Haule enzi za uhai wake. Wataalamu wa afya akiwemo Dk. Mandai A. Mandai wa hospitali ya Temeke ambaye alitaja sababu zinazosababisha wasanii wengi kufariki: 
1. KUKOSA TABIA YA KUPIMA AFYA MARA KWA MARA
Wasanii wengi wa Kibongo hawana utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara. Wengi huenda hospitali wakiwa tayari wanaumwa na matokeo yake, hata yale maradhi ya kawaida ambayo yangeweza kutibika mapema na kupona, yakiwemo malaria, kifua kikuu na mengineyo, huwasababishia vifo. 

2. MTINDO WA MAISHA
Mtindo wa maisha ya mastaa wa Kibongo unashangaza sana. Wengi wanakesha kwenye kumbi za starehe wakinywa pombe kali, kuvuta sigara na kufanya ngono, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao huku wakisahau kabisa kumcha Mungu wao. 

Wengi hawapati muda wa kutosha wa kulala na kupumzisha miili yao, hawali chakula bora wala hawafanyi mazoezi ya mwili, matokeo yake, wakipatwa na maradhi hata yale ambayo ni ya kawaida, kinga za miili yao zinakuwa chini na kusababisha wapoteze maisha.


Marehemu Steven Kanumba enzi za uhai wake. “Ili mwili wa binadamu uwe na afya bora, mtu anapaswa kulala kwa saa zisizopungua nane kila siku, kunywa maji mengi, kula chakula bora, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi makubwa ya pombe na uvutaji sigara,” Dokta A. Mandai wa Hospitali ya Temeke ameliambia Ijumaa. 

3. MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA
Hili ni janga lingine linalowapukutisha wasanii wengi Bongo. Albert Mangwea ‘Ngwair’, Langa Kileo, Aisha Madinda, Malick Ahmed ‘Mack 2B Simba’, Ahmed Ally Upete ‘Geez Mabovu’ na wengine wengi, ni miongoni mwa wasanii ambao kwa namna moja au nyingine, vifo vyao vimechangiwa kwa kiasi kikubwa na madawa ya kulevya. 

Bado idadi ya wasanii wengine wanaoendelea kutumia madawa hayo hatari ni kubwa na kama jitihada za haraka hazitatumika kuwanusuru, huenda nao wakapitia njia hiyohiyo (japo hatuombei itokee). 

4. AJALI ZA BARABARANI
Dairekta maarufu na msanii wa filamu Bongo, George Tyson, kifo chake kilisababishwa na ajali ya gari na kuacha simanzi kubwa kwenye tasnia ya filamu. Hali kadhalika msanii Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’, naye maisha yake yalikatizwa na ajali mbaya ya gari iliyotokea Muheza, Tanga.Naye Abuu Semhando, aliyekuwa mpiga drums wa Bendi ya Twanga Pepeta, alifariki kwa kugongwa na gari akiwa anaendesha pikipiki, maeneo ya Mbezi Beach.