Monday, June 29, 2015

NDOA YA OKWI YATIKISA UGANDA, YAHUDHURIWA NA VIONGOZI WA KIJESHI

Mchezaji wa Simba, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda,akiwa na mke wake, Nakalega Florence katika pozi.
NDOA ya mchezaji wa Simba, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda, aliyofunga na Nakalega Florence, juzi Jumamosi kwenye Kanisa la Lubaga Miracle Center, linaloongozwa na Mchungaji Robert Kayanja, ilionekana kutikisa viunga mbalimbali vya Jiji la Kampala nchini hapa.
Kutikisa kwa ndoa hiyo kulitokana na vyombo mbalimbali vya habari kuitangaza ndoa hiyo mara kwa mara hasa siku yenyewe ya tukio.
Utaratibu wa ibada ya ndoa hiyo ulianza saa saba kamili mchana ambapo waumini na watu wote waliofika kanisani walisachiwa wao na vitu walivyobeba kwa kutumia kifaa maalum na kisha kupitishwa sehemu nyingine ya kuukagua mwili wote zoezi ambalo lilisimamiwa na askari polisi waliokuwa na silaha.
Baada ya kufunga ndoa kanisani hapo, msafara wa maharusi hao ukiongozwa na gari tano za kifahari aina ya Jaguar toleo namba 300C na kufuatiwa na magari mengine, ulielekea Munyunyu Resort Beach iliyopo kando ya Ziwa Victoria kwa ajili ya zoezi la upigaji picha za mapozi.
Mpiga picha Mkuu wa Global Publishers, Richard Bukos akiwa katika picha ya Pamoja na wana ndoa hao.
MSAFARA WA MAHARUSI WAPATA AJALI
Hata hivyo, sherehe hizo zilitaka kuingia simanzi baada ya gari walilopanda wasimamizi wa maharusi hao (Bestman na Matroni) Hamis Kiiza na Nabisubi Julian kugongwa kwa nyuma na gari lililokuwa likiendeshwa na Meneja wa Okwi, Baker Bawe, hivyo yote kubonyea.
Kutokana na ajali hiyo, msarafa huo ulisimama kwa muda lakini kwa kuwa magari hayo yalikuwa kitu kimoja, tukio hilo halikuchukua muda mrefu na magari hayo yaliendelea na safari yakiwa na muonekano mbaya wa ajali.
Msafara huo uliendelea mpaka Ukumbi wa Uma uliopo Lugogo nje kidogo ya Jiji la Kampala ambapo ndani yake kuna ukumbi mkubwa uitwao Main Exhibition ndipo mambo shamrashamra na vigeregere vya Kiganda viliendelea.
KIGOGO WA JESHI LA UGANDA ATOA NASAHA
Sherehe hizo zilihudhuriwa na kiongozi wa kijeshi nchini Uganda aliyefahamika kwa jina la Brigedia Hassan pamoja na askari wengine ambapo kigogo huyo aliwapa nasaha maharusi hao. Ulipofika wakati wa kutoa shukrani pamoja na mambo mengine, Okwi alilishukuru jeshi la nchi hiyo kwa kampani kubwa kwenye harusi yake.
Pamoja na viongozi wa kijeshi, walikuwepo viongozi mbalimbali wa Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa) ambao waliwakilishwa na rais wa shirikisho hilo, Moses Mabuku.
Kocha Mkuu wa Uganda ‘The Cranes’, Milutin Sredojević ‘Micho’ na msaidizi wake, Moses Basena aliyeambatana na mkewe, Salome Basena nao walionekana wakitafuna vipapatio vya kuku, ndizi kama zile za Bukoba, tambi, chapati, wali maua, wali mweupe, pilau na mapochopocho mengine yaliyotengenezwa kiufundi.
Sherehe hizo zikiendelea, wazazi wa Okwi, mzee Anord Okwi na mama Okwi, Ajiyo Grace walikuwa wakitumia muda huo kuwashukuru wageni mbalimbali waliohudhuria kwenye hafla hiyo ambapo walishindwa kuficha hisia zao na kurukaruka kwa furaha kila mdundo wa muziki ulipowakolea.
Kama ilivyo katika harusi nyingine licha ya wazazi wa Okwi ndugu aliozaliwa nao katika familia hiyo ya baba mmoja yenye watoto watano wakiongozwa na Emmanuel Okwi, Caroline, Martin, Olaki Francis na kitinda mimba wao Morine, wote walijumuika kuserebuka kwenye mnuso huo.