Sunday, June 28, 2015

UGONJWA WA BANZA UNAWAUMIZA VICHWA MADAKTARI, HALI MBAYA

banzaMwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ akiugulia.
Gladness mallya
INASIKITISHA sana! Wakati hali ya afya ya mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ ikiwa ni mbaya nyumbani kwao Sinza jijini Dar es Salaam, madaktari wanapata tabu na kusumbuka kuhusu ugonjwa wa fangasi ya kichwa unaomsumbua.
Licha ya ugonjwa huo, pia kwa mujibu wa ndugu wa karibu, hivi sasa Banza pia anasumbuliwa na tatizo la maumivu makali wakati wa kupata haja ndogo, kiasi kwamba hupiga kelele anapofanya hivyo, huku akiwa pia haoni wala kusikia vizuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini hivi karibuni, baadhi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya kichwa wamesema ugonjwa wa kichwa wa Banza, ambao kitaalamu huitwa Mucormycosis, husababishwa na fangasi waitwao Murcorales ambao huingia ndani ya mwili wa binadamu kwa njia ya hewa.
“Ingawa ugonjwa huu ni hatari, lakini unatibika, ukivuta hewa yenye fangasi hao, huingia na kwenda moja kwa moja kwenye mfumo wa damu kisha kuanza kuzunguka ndani ya mwili kufuata damu. Baada ya kukaa kwa wiki kadhaa kwenye mfumo wa damu, huhamia kwenye uti wa mgongo (spinal) ambapo huzaliana kwa wingi na kuanza kusambaa kuelekea kwenye ubongo,” alisema dokta mmoja wa hospitali moja kubwa jijini Dar.
Daktari mwingine wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema ugonjwa unaomsumbua Banza ni hatari kwani mashambulizi yake huwa ni makubwa na husambaa kwa kasi kiasi kwamba wagonjwa wanaougua huwa na hali mbaya.
“Kati ya wagonjwa 100 wanaoumwa ugonjwa huu, 30 hupoteza maisha,” alisema kwa kifupi daktari huyo akiuzungumzia ugonjwa unaomsumbua nyota huyo ambaye yupo kitandani kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, akipatiwa matibabu katika hospitali ya Sinza-Palestina na kurejea nyumbani kwao.
Jumatano iliyopita, wadau mbalimbali wa muziki walimiminika nyumbani kwao baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa mtunzi huyo hodari alikuwa amefariki dunia, ikiwa ni zaidi ya mara kumi akizushiwa jambo hilo.