Wednesday, June 10, 2015

VILIO VYATAWALA VIFO VYA PADRI WANAFUNZI SITA

VILIO na simanzi vilitawala  mazishi ya Padri Hyasint Kawonga na baadhi ya  wanafunzi walioteketea kwa moto wilayani Mbinga mkoani Ruvuma baada ya ajali ya gari iliyotokea hivi karibuni.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, John Ndimbo.
“Ni msiba uliokusanya mamia ya waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini wilayani hapa, inauma sana.”
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, John Ndimbo wakati alipokuwa akiongoza ibada ya mazishi ya padri huyo yaliyofanyika Jumamosi aliyefariki dunia kwenye ajali hiyo na wanafunzi sita, huku majeruhi 24 wakikimbizwa hospitali.
Askofu Ndimbo alisema katika kipindi hiki cha maombolezo, kuna kila sababu ya waumini wa Kikristo kuendelea kuwaombea marehemu hao kwa kusali na kumuomba Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi.
Hadi juzi majeruhi 20 walikuwa wameruhusiwa kurudi nyumbani, lakini wanne bado wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Wanafunzi waliofariki dunia walikuwa wanasoma katika Shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) iliyopo katika Kata ya Kigonsera na Padri Kawonga alikuwa ni mkurugenzi wa shule hiyo pia Paroko wa Kigonsera  jimboni humo na ndiye alikuwa dereva wa gari lililopata ajali lenye namba za usajili T 306 AYM aina ya Land Rover 10 liliposhindwa kupanda mlima.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo viongozi wa dini na serikali, mwili wa marehemu Kawonga umezikwa katika Makaburi ya Parokia ya Kigonsera wilayani Mbinga.Kadhalika nao wanafunzi waliofariki dunia, Fidea Ndunguru (17) na Suzan Kawonga (17) wote wa kidato cha nne miili yao ilisafirishwa kwenda katika Kijiji cha Mpapa wilayani Mbinga kwa ajili ya mazishi.
Wengine wawili walisafirishwa kwenda makwao ambao ni wa familia moja ni kutoka Kijiji cha Namabengo wilayani Namtumbo, ambao ni Gladness Ngonyani (17) na Kelvin Ngonyani (20) na kwamba Damas Mbele (16) wa kidato cha pili kutoka Kijiji cha Myangayanga na Philoteus Hyera (16) wa Kijiji cha Mahenge wilayani Mbinga nao walisafirishwa kwenda nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi.
Awali kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Mihayo Msikhela, ajali hiyo ilitokea Juni 4, mwaka huu majira ya jioni, wakati wanafunzi hao na Padri Kawonga walipokuwa wakitoka shambani kuvuna mahindi yaliyokuwa yamelimwa kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo.