Thursday, June 11, 2015

WAZIRI WA ELIMU ASHINDWA KUMALIZA MGOGORO WA CHUO KIKUU KAMPALA BAADA YA KUKIRI UDHAIFU,CHUO CHAFUNGWA

Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Dk Shukuru Kawambwa ameshindwa kutatua mgogoro wa wanafunzi wa kozi ya famasia wa chuo kikuu cha Kampala na kudai kuwa hadi akakutane na waziri wa afya.
Dk Kawambwa amekwenda chuoni hapo kwa lengo la kuzungumza na uongozi wa chuo pamoja na wanafunzi kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo ambapo mbali na kukiri kuwa kuna taasisi ambayo haikufanyakazi yake inavyopasa hadi hayo yakatokea amesema serikali itatoa tamko juu ya hatma ya wanafunzi waliomaliza kozi hiyo na vyeti vyao kutokutambuliwa kwenye ajira.
 
Kwa upande wake katibu mtendaji wa TCU Prof Yunuth Mgaya amesema bodi yake haihusiki na mgogoro huo na kwamba chuo hicho kimesajiliwa na kipo nchini kisheria huku akiwatoa hofu wazazi wenye watoto wao chuoni hapo.
 
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kikao cha waziri akiwemo waziri wa elimu wa chuo hicho Answari Mnyonge amesema wanafunzi wako tayari kurudi madarasani pale tu usajili utakapokamilika huku afisa habari wa KIU akielezea athari zilizotokana na vurugu zilizotokea hivi karibuni chuoni hapo.
 
Hata hivyo licha ya wanafunzi hao kutakiwa kuondoka chuoni hapo baada kutangaziwa kuwa kimefungwa lakini bado wameendelea kuwepo kushinikiza utatuzi wa mgogoro huo huku askari wa kikosi cha kituliza ghasia FFU wakiendelea kuimarisha ulinzi chuoni hapo.