MADEREVA nchini wametishia kufanya mgomo kwa mara nyingine kuanzia wiki ijayo na kwa muda usiojulikana iwapo serikali kupitia kamati iliyoundwa kushughulikia matatizo yao haitawaita na kuongea nao kuhusu posho zao za ndani na safari za nje.
Kauli hiyo imetolewa jijini dar es Salaam jana na Katibu mkuu wa Chama cha Madereva, Rashid Salehe ambapo alisema madereva hao wamemtuma na kuitaka serikali isimuulize kiongozi yeyote wa madereva kipindi watakapoamua kugoma mpaka madai hayo yatekelezwe.
Alisema kuwa pamoja na kupata mikataba mipya katika kikao cha mwisho kilichofanyika mwezi uliopita hata hivyo bado madereva wanaendelea kupewa mikataba mingine tofauti na ile waliokubaliana katika kikao hicho cha mwisho.
“Madereva bado wanaendelea kupata shida na kusota bila kujua hatima ya posho zao za safari za ndani na nje hivyo tunaitaka Wizara ya mambo ya Ndani na Wizara ya Kazi isije kutuita viongozi na kutuuliza juu ya hili kwa kuwa madereva hao wamechoka hivyo wamenituma baada ya kufanya ziara za mikoa kadhaa na kuniagiza niseme kuwa wataacha kuendesha magari kama serikali haitawaita kujua hatima ya suala hilo” alisema Salehe.
Aliongeza migogoro kati ya madereva na matajiri wa magari hayo ni kutokana na mfumo wa viongozi wa serikali kuhusika kuwafanya biashara hiyo huku wakiwa wanawakandamiza waliochini.
“Kuna kampuni ya magari fulani sitayataja jina tajiri wake analugha za matusi na tumeshamrekodi wakati akitoa matusi hayo na tunafikiria kumpeleka huyu bwana mahakamani” alisema Salehe.
Alisema kuwa pia kuna gari la kigogo mmoja ambalo lilibeba sumu za mgodini limekwama porini muda mrefu na tajiri wa basi hilo amewatelekeza madereva hao bila kujali afya zao zinaendelea kuharibika kwa kukaa na sumu hiyo.
Salehe alisisitiza kama mfumo uliopo wa vigogo wa sarikali kuwa ndio wamiliki wa mabasi hayo basi kila watakalo kuwa wanafanya litaonekana la kitoto na migogoro haitaisha na ukizingatia wanalindwa na sheria ya mwaka 1955 ambayo wanaitumia mpaka leo.