Tuesday, August 11, 2015

Denti alazwa, kisa viboko shuleni

FIMBO (4)Kabula Wilson akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Pwani, Tumbi.
Deogratius Mongela na Chande Abdallah
KATIKA hali isiyo ya kawaida mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, Kabula Wilson (18), alipoteza fahamu kisha kukimbizwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Pwani, Tumbi, kwa madai ya kucharazwa bakora na walimu wake kisa, kukamatwa barua ya kuwatukana.
FIMBO (1)Tukio hilo linadaiwa kujiri Agosti 6, mwaka huu, katika ofisi ya walimu shuleni hapo ambapo baadhi ya wanafunzi wa vidato mbalimbali walikuwa wakiitwa kwa makundi na kuulizwa ni nani aliyeandika barua  hiyo, lilipokosekana jibu inadaiwa walimu hao kila mmoja kwa wakati wake aliwachapa wanafunzi hao bila kuangalia eneo sahihi ikiwa pamoja na kichwani, mgogoni, miguu na katika maeneo mengine nyeti.
Kwa mujibu wa dada wa mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Magreth Wilson,  Jumatano, Agosti 5, Kabula alirudi nyumbani akiwa amevimba mwili mzima na kushindwa kula kwa madai ya kupigwa na walimu na alipomuuliza kisa cha kuchapwa alidai kuwa kuna barua ya matusi iliokotwa na walimu shuleni kwao hivyo wanamtafuta aliyeiandika.
FIMBO (2)Alisema kuwa alipomuuliza kwa nini achapwe kiasi hicho kwani yeye ndiye mhusika,  akajibu kuwa hahusiki lakini  walimu waliwachapa wanafunzi wote wa madarasa ya juu.
 “Mama yake alimpa dawa lakini alikataa kula na kulala na njaa kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyasikia na asubuhi yake alienda shule licha ya kuwa na maumivu,” alisema Magreth.
Huku akiongea kwa masikitiko akaongeza kuwa tabia hiyo ya walimu wa shule hiyo imekuwa siyo mara ya kwanza kwa kuwachapa wanafunzi mpaka kuzimia.
FIMBO (3)Kwa mujibu wa chanzo chetu na mashuhuda mbalimbali wa tukio hilo, walisema zoezi la kuwachapa wanafunzi hao lilianza Agosti 5, mwaka huu ambapo kila mwanafunzi alichapwa na zaidi ya walimu sita huku wakiwalazimisha wamtaje aliyeandika barua hiyo lakini siku hiyo hawakumtaja ndipo likaendelea siku iliyofuata.
Siku iliyofuata walimu wakati wanawachapa wanafunzi tena, ndipo Kabula na wenzake wawili walizimia kwa kuzidiwa na bakora huku walimu wakisema walijifanyisha na kuwaamuru wenzao wawatoe nje ya ofisi.
Kutokana na hali ya wanafunzi hao kuwa mbaya hasa Kabula, iliwalazimu wanafunzi wachange pesa ili wamkimbize Hospitali ya Tumbi.
Walimu walipoona hali inazidi kuwa mbaya waliwatawanya wanafunzi kisha wakampeleka Kabula katika hospitali hiyo na kuandika maelezo ya uongo ili kukwepa skendo hiyo.
“Kitendo hicho kimetuumiza tunaiomba serikali kufuatilia mara moja ili wanafunzi waliopatwa na matatizo wapate haki zao kwani ni zaidi ya wanafunzi watatu walizimia.
 “Kama familia tunapinga vikali sana unyama huu, Kabula hali yake haipo sawa mpaka sasa analalamika kuwa na maumivu na mbaya zaidi hakuna mwalimu aliyefika kumjulia hali.
 “ Tumeshatoa taarifa polisi na askari walifiki shuleni kwa lengo la kuonana na Mwalimu Mkuu, Felister ambaye inasemekana hakuwepo tangu lilipotokea tukio hilo,” alisema Magreth.
Baada ya taarifa hizo gazeti lilimpigia simu mmoja wa walimu wa sekondari hiyo aliyejitambulisha kwa jina la George Ngonyani ambaye alikiri kuwepo kwa tatizo hilo lakini akasema yeye siyo msemaji wa shule.
Mwalimu mkuu hakupatikana lakini afisa mmoja wa Kituo cha Polisi Kibaha ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema wanachunguza.