Tuesday, September 8, 2015

JK ATEMBELEA MAJERUHI MKUTANO WA KAMPENI WA DK. MAGUFULI MORO.

Katika tukio hilo watu wawili walipoteza maisha na 19 kujeruhiwa.

Rais Jakaya Kikwete, amewatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya  kukanyagana wakati wakitoka kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo kusikiliza mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ambapo watu wawili walipoteza maisha na 19 kujeruhiwa.
 
Rais Kikwete ambaye alihuduhuria mkutano huo wa kampeni katika uwanja huo juzi, alifika hospitalini hapo jana akiwa amefuatana na mkewe wake, Mama Salma Kikwete na kutoa pole kwa majeruhi hao na wafiwa.
 
Akizungumza hospitalini hapo, Rais Kikwete alisema amehuzunishwa na tukio hilo na kutaka liwe fundisho kwa mikutano mingine inayoendelea ya kampeni hasa kunapokuwa na msongamano mkubwa wa watu.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Rita Lyamuya, alisema walipokea majeruhi 19 na miili ya watu wawili waliofariki katika tukio hilo, Grace George (42) na mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mkundi, Ranmadhani Abdalah (12).
 
Alisema majeruhi hao wameumia maeneo ya miguu, mikono, vifua na wachache kati yao kuvunjika viungo mbalimbali vya mwili na kuchanika na kwamba saba walitibiwa na kuruhusiwa, huku 10 wakiendelea na matibabu hospitalini hapo na hali zao zinaendelea vizuri.
 
Akizungumza baada ya kupata maelezo hayo, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine aliushauri uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na serikali kupanua hospitali hiyo kwa kujenga majengo ya ghorofa ili iweze kuchukua wagonjwa zaidi ya 450 wanaopatiwa matibabu kwa siku kwa sasa.

Tulizungumza na baadhi ya majeruhi waliokuwa wakipata huduma hospitalini hapo na mmoja wao Mariam Mkunda alisema kilichosababisha ni vibaka waliotumia nafasi ya kukosekana kwa ulinzi baada ya kuondoka msafara wa Magufuli na Rais Kikwete.
 
Alisema vibaka hao walifunga lango kuu la uwanja wa Jamhuri kwa nia ya kupora watu na  askari wachache walipofika na kufungua lango hilo watu walisukumana, kuangushana, kukanyagana, kupoteza fahamu, kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha.
 
Pia lilifika nyumbani kwa marehemu Grace katika kata ya Kilakala na kukuta umati mkubwa wa watu umejitokeza kwa ajili ya msiba huo, ambapo ndugu jamaa na marafiki walieleza kupokea kwa masikitiko kifo hicho cha ghafla cha mpendwa wao ambaye alikuwa ni kada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi.