Friday, September 25, 2015

ACT- Wazalendo Yalia na Ukata wa Fedha za Kampeni


Wakati zikiwa zimebaki siku 29 kuelekea uchaguzi mkuu, kampeni za mgombea urais wa chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira zinakabiliwa na uhaba wa fedha ambazo sasa zimebaki Sh. milioni mbili tu.

Tangu mgombea huyo alipozindua kampeni zake Agosti 30, mwaka huu hadi sasa, chama hicho kimeshatumia Sh. milioni 363 ambazo ni wastani wa takribani Sh. milioni 15 kwa siku.

Lakini kutokana na ukata unaokikabili, kwa sasa kinalazimika kutumia Sh. 66,667 kwa siku.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na Kampeni Taifa wa ACT-Wazalendo, Nixon Tugara, juzi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, kutokana na changamoto wanayokabiliana nayo ya uhaba wa fedha anatoa wito kwa Watanzania popote walipo kuchangia kampeni za chama hicho.

“Mtu anaweza kutoa kiasi chochote na tutashukuru sana kwa ushirikiano wa kuijenga Tanzania yenye misingi ya haki...chama chetu kinakabiliwa na wakati mgumu kifedha, tumekuwa tukijitahidi kuzunguka sana kutafuta fedha kwa marafiki zetu na kuchangishana miongoni mwa wanachama lakini hatujafikia lengo letu la kiwango tunachohitaji cha fedha za kufanya kampeni bora”