MAPEMA saa za jioni, makundi ya wakazi wa Moshi yalimiminika kwenye Uwanja wa Majengo kwenda kushuhudia tukio lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa, onyesho la Serengeti Fiesta. Kwa kuwa hata mwaka jana lilifanyika hapa, mashabiki walifahamu fika ni nini cha kutarajiwa haswa katika ubora, lakini safari hii kukiwa na kitu kingine tofauti.
Kampuni ya Bia ya Serengeti, kupitia kinywaji chake, Serengeti Premium Lager, kwa kushirikiana na waandaaji, Prime Time Promotions, walihakikisha kwamba mashabiki wanapata burudani ya nguvu hadi majogoo.
Kazi kubwa iliyofanywa jukwaani na wasanii kama Mh. Temba ambaye ni mwenyeji wa Moshi, Ali Kiba, Ney wa Mitego, Dully Sykes, JamboSquad, Stamina, Maua, Recho na Sha haikuwapa mashabiki nafasi ya kupumua katika onyesho hilo lililoanza saa mbili asubuhi hadi asubuhi ya siku iliyofuata.
Ali Kiba aliwathibitishia mashabiki kwamba yeye ni moto wa kuotea mbali pale alipowafanya mashabiki hao kuimba pamoja naye baadhi ya nyimbo zake kama ‘Mwana Dar es Salaam’, ‘Kimasomaso’,’ mapenzi yana-run dunia’ na ule maarufu zaidi, ‘dushelele’.
Mpangalio wa matukio ulikuwa na ubora mkubwa huku mashabiki kutosubiri kwa muda mrefu kwenye foleni wakati wa kuingia uwanjani, kitu tofauti kabisa na maonyesho mengine. Kitu kipya kwenye shoo hiyo kukaribishwa kwa akina mama lishe wa kutosha kwa ajili ya kutoa huduma ya chakula.
”Tuligundua kwamba si kila mtu anapenda kula kile chakula cha kawaida kwenye shoo nyingi, nyama choma na chipsi, ndio maana tukaamua kuwaita na hawa mama lishe kuja kuuza chakula hapa,” alisema Rodney Rugambo, Meneja wa Serengeti Premium Lager.
“Tumekuwa tukisisiiza kwamba tunataka kuwawezesha watu wa kawaida na hii ni moja kati ya juhudi hizo, na tunatarajia kufanya hivyo katika mikoa mingine iliyosalia tutakakokwenda kufanya maonyesho,” aliongeza.
Mbali na shoo hiyo, kulikuwa na shughuli nyingine kadhaa zilizofanyika, kama vile bonanza la soka, ‘Dance la Fiesta’ ambapo washindi hupewa nafasi ya kutembelea Dar es Salaam kushuhudia shoo ya mwisho itakayofanyika Oktoba 18 mwaka huu.
Moshi, mji uliopo chini ya Mlima Kilimanjaro, unahitimisha wiki ya nne ya ziara hii inayotarajiwa kufanyika katika mikoa 14 zaidi nchini; na wikendii ijayo itakuwa ni zamu ya Musoma.