Mtanzania mmoja aliyefahamika kwa jina la utani la Mabastola, amefariki dunia jijini Istanbul nchini Uturuki mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kumrusha mwanaye kutoka katika ghorofa ya tatu ya jengo alilokuwa akiishi kisha na mwenyewe kujirusha na kufa papo hapo.
Chanzo chetu kilichopo jijini humo, kimeliambia gazeti hili kuwa kinacho taarifa za msiba huo ambao chanzo chake halisi hakijafahamika, lakini kitendo cha marehemu huyo kumtupa mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka kumi, kinaonesha alikuwa na tatizo la kisaikolojia.
“Ninamfahamu marehemu na hilo tatizo lipo, kabla hajajirusha mwenyewe, kwanza alimtanguliza mtoto wake ambaye alifia hospitalini na tunamzika leo saa saba (Jumatatu). Marehemu bado hatujajua kama tutamhifadhi hapa au tutamrejesha nyumbani,” alisema mtoa habari huyo.
Alisema kuna gharama kubwa za kuusafirisha mwili kutoka Uturuki hadi Tanzania na kwa sababu hiyo, Watanzania walioko huko wanapeana taarifa ili kuona kama wanaweza kutoa michango itakayotosha au la.
Kuhusu wasifu binafsi wa marehemu, chanzo hicho kilisema marehemu alikuwa akiishi na mwanamke mwenye uraia wa Uturuki, lakini hakuwa na asili ya nchi hiyo, akishindwa kuthibitisha asili hasa ya mkewe huyo na kuhusu kazi, alisema Mabastola hakuwa na kazi rasmi kwani alikuwa mtu wa kujichanganya katika mihangaiko ya maisha.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, jitihada za kufahamu sehemu anayotokea Mabastola nchini Tanzania hazikuwa zimefanikiwa.